Maoni: COP26 ni kikombe nusu na sio nusu kikombe
15 Novemba 2021Je, mkutano wa hivi punde mjini Glasgow ulikuwa mzuri ama mbaya? Majibu ya swali hili yametafautiana kwa namna ile ile ambapo mkutano wenyewe ulikuwa na tafrani na mashaka.
Wanasayansi wanasema, haijawahi kutokezea hapo kabla kukawa na pengo kubwa baina ya hatua muhimu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kasi ndogo za mataifa kama ilivyo sasa.
Lakini pia shinikizo la kuwataka kuchukuwa hatua ni kubwa zaidi kuliko ilivyowahi kuwa. Vuguvugu la Ijumaa kwa Mustakabali ambalo linapigania ulinzi wa mazingira lilijidhihirisha lilivyo na nguvu mjini Glasgow.
Tamko zito, lugha nyepesi
Tamko la mwisho kutoka mkutano huo, likiwa la kwanza la aina yake kutoka mkutano wowote kama huu wa Umoja wa Mataifa, linaoneshea kwa kina kabisa umuhimu wa kuachana haraka na vyanzo vya nishati ya visukuku, hata kama njia lilivyoandikwa tamko hilo limepozwa mno ili kuyaridhisha mataifa tajiri na mataifa mapya ya viwanda.
Mataifa masikini yameahidiwa kwamba msaada wa kifedha kutoka mataifa tajiri ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi utaongezwa maradufu ndani ya miaka michache ijayo.
Baada ya miezi kadhaa ya uhusiano wa mashaka, Marekani na China, ambayo ndiyo mataifa yanayozalisha gesi chafu kwa wingi zaidi ulimwenguni, ziliungana na kutoa tamko la pamoja zikiahidi kuongeza juhudi zao.
Lengo la kuzuwia sayari ya dunia isipate joto zaidi ya nyuzi 1.5, juu ya kiwango kilichokuwapo kabla ya mapinduzi ya viwanda, kabla ya mwishoni mwa karne hii, sasa ndicho kipimo cha mambo yote: sasa hakuna anayezungumzia tena lengo la nyuzijoto 2 lililokuwa kiini cha mijadala ya mwanzoni juu ya sera ya mabadiliko ya tabianchi.
Maazimio yasiyolazimisha kufuatwa
Kwa hakika, haya yalikuwa maendeleo ya kutia moyo sana kwa mintarafu ya maazimio yaliyofikiwa kwenye mikutano ya awali ya mabadiliko ya tabianchi.
Lakini si kwa mintarafu ya ukweli unaotukabili sasa. Wanasayansi wanasema muongo huu kuelekea mwaka 2030 ndio utakaomuwa hatima ya mapambano dhidi ya kupanda joto la sayari ya dunia.
Wenyeji wa mkutano huu, Uingereza, walikuja na orodha ya hatua chungu nzima ambazo mataifa yaliyokuwepo Glasgow yanafanywa kuzichukuwa: kuzuwia uzalishaji wa gesi ya methane, kuilinda misitu ya mataifa masikini, kukomesha ruzuku kwa nishati za visukuku - na yote hayo kabla ya mwaka 2030.
Hata hivyo, ukiyachunguza kwa undani, yote haya yanaonekana ni mambo ya hiyari na hayazifungi serikali za mataifa hayo kuyafuata - kama yalivyo maazimio yote yaliyowahi kutangazwa na mikutano mingine ya mabadiliko ya tabianchi.