1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Hatari kubwa kwa Wayahudi nchini Ujerumani

Daniel Gakuba
10 Oktoba 2019

Waumini katika Sinagogi mjini Halle mashariki mwa Ujerumani waliponea chupuchupu kukumbwa na mauaji ya halaiki, yaliyopangwa na Mnazi mamboleo kwenye siku kuu ya dini yao. Chuki dhidi ya Wayahudi haipaswi kubezwa.

https://p.dw.com/p/3R1cX
Deutschland Halle nach Anschlag auf Synagoge
Picha: picture-alliance/dpa/J. Woitas

Wanaume na wanawake zaidi ya 70 walikuwa wamekusanyika katika sinagogi hilo la kiyahudi kusali na kuimba katika maadhimisho ya siku kuu ya Yom Kippur. Kilichomzuia kumwaga damu nyingi muuaji huyo aliyejihami kwa bunduki na guruneti ni mlango wa sinagogi  uliotengenezwa maalum kuhakikisha usalama.

Hayo yalitokea tarehe 9 Oktoba 2019. Miaka 80 baada ya vita vikuu vya pili vya dunia ambapo Wayahudi milioni 6 waliangamizwa, na sasa, Wayahudi wanalazimika tena kuhofia usalama wa maisha yao, pale wanapokusanyika katika ibada kulingana na imani yao.

Hali hiyo inaipa sura gani Ujerumani? Na inamaanisha nini kwamba mwanamme mwenye umri wa miaka 27 alipata hadhara ya kumtazama, aliporusha moja kwa moja kitendo chake cha mauaji kwenye jukwaa la michezo ya video mtandaoni?

Shambulizi lilionyesha mtandaoni

Kama ilivyotokea mjini Christchurch-New Zealand, kabla ya kuanza mashambulizi, alijipiga picha mwenyewe akituma ujumbe kwa watumiaji wa mtandao wa kimataifa, pale alipozungumza kwa lugha ya Kiingereza akisema ''Mzizi wa matatizo yote ni Wayahudi''.

Ines Pohl Kommentarbild App
Ines Pohl, Mhariri Mkuu wa DWPicha: DW/P. Böll

Rambirambi zetu zinapaswa kuelekezwa kwanza kwa familia za mwanamke na mwanamme waliouawa kinyama na mshambuliaji. Lakini pia hatupaswi kufumbia macho ukweli kwamba, hali ingekuwa tofauti kidogo, tungeshuhudia mauaji ya halaiki ya Wayahudi ndani ya Ujerumani jana Jumatano.

Chuki hii haiishi tu katika makundi ya kiislamu

Mashambulizi ya jana yanathibitisha kwamba kuongezeka kwa chuki dhidi ya Wayahudi katika nchi hii hakuishii tu miongoni mwa magaidi wafuasi wa itikadi kali ya Kiislamu. Yeyote anayeshikilia madai hayo ni mwongo asiyetaka kukabiliana na ukweli.

Mkasa huu unadhihirisha kwamba bado ni muhimu kuzipatia ulinzi taasisi za Kiyahudi, hata leo, karibu miaka 75 baada ya kumalizika kwa utawala dhalimu wa Wanazi. Hali ya kwamba nyumba ya ibada ya Kiyahudi haikupatiwa ulinzi kwenye siku kuu ya Yom Kippur, inazua maswali mengi.

Uhalifu huu ni ushahidi kwamba hata kidokezo kidogo tu cha chuki dhidi ya Wayahudi kinapaswa kupewa uzito na kuchunguzwa, vikiwemo vile vya kuchoma bendera ya Israel au kuwatukana watu wanaovaa alama za dini yao kama kikofia cha yarmulke.

Chuki dhidi ya Wayahudi haipaswi kubezwa. Hakuna kitu kama kiasi kidogo cha chuki ya aina hiyo, na hususan nchini Ujerumani.