Maoni juu ya Waziri Mkuu Erdogan
27 Desemba 2013Katika maoni yake mwandishi wetu Baha Güngör anahoji kwamba sasa suala siyo tena , iwapo Waziri mkuu huyo na baraza lake la mawaziri watajiuzulu, bali swali ni lini Erdogan atalikata jongoo kwa meno?
Yalitokea nchini Uturuki sivyo alivyotaka Waziri Mkuu Erdogan kuumaliza mwaka huu .Badala ya ustawi wa uchumi wa kiwango cha kuonewa kijicho ,sarafu imara na kuzidi kujengeka kwa ushawishi wa Uturuki kikanda, maji yamemfika shingoni waziri Mkuu Erdogan. Swali sasa siyo tena iwapo yeye na baraza lake la mawaziri watajiuzulu bali ni lini waziri Mkuu Erdogan ataufungua mwavuli na kuchupa!
Alikuwa hana wasi wasi bungeni
Mwenyekiti huyo wa chama cha Haki na Maendeleo, AK kinachoiongoza serikali ya Uturuki mpaka sasa amekuwa anategemea wingi aliokuwa nao bungeni kiasi cha kufikia hatua ya kutikisa miguu katika bunge hilo-ameakuwa anafanya hivyo tokea ushindi wake wa kwanza katika uchaguzi wa mwaka wa 2002.Tokea wakati huo hajakabiliwa na upinzani wowote wa kumshtua.Ameweza kupanga na kupangua jinsi alivyopenda.
Hana stahamala
Lakini Waziri Mkuu Ergodan amefanya makosa kama jinsi wanavyofanya viongozi wengine wanaotawala peke yao. Alifikiri kwamba yeye hawezi kukosea.Erdogan hakuvumilia kukosolewa ,waliokuwa na mitazamo tofauti,kama vile waandishi wa habari, wasomi na wanasiasa walijikuta vizimbani. Na hata idadi kubwa ya viongozi wa jeshi wa hapo awali walitiwa ndani kwa madai kwamba walifanya matayarisho ya kuiangusha serikali.Majerali hao walipewa adhabu ya vifungo virefu jela.
Rushwa isiyokuwa na kifani
Erdogan alianza kujibomoa mwenyewe katika miezi ya hivi karibuni.Jinsi alivyokabiliana na watetezi wa demokrasia na wawakilishi wa asasi za kiraia,ilithibitisha jinsi alivyokuwa na wasi wasi .Alichukua hatua za kikatili dhidi ya raia waliokuwa waandamana kuupinga mpango wa ujenzi kwenye bustani ya mapumziko katika mji wa Istanbul.
Mishipa ya fahamu ya Waziri Mkuu Erdogan ilishindwa kufanya kazi baada ya polisi na mahakama kuifichua kashfa kubwa ya rushwa isiyokuwa mithili katika historia ya miaka 90 ya Uturuki. Baada ya uchunguzi wa rushwa kufika hadi katika maskani yake ya kibinafsi, amejaribu kuukimbia ukweli .Madai mazito ,juu ya wizi wa dhahabu,uekezaji wa fedha haramu ,hongo kwa ajili ya kupatiwa kandarasi za ujenzi na biashara haramu ya kibenki na Iran .Madai hayo yamemgusa Waziri Mkuu Erdogan
Alibadilisha Baraza la mawaziri
Amebadilisha baraza lake la mawaziri.Lakini hilo siyo suluhisho. Lakini ikiwa Erdogan ataanguka kutokana na msimamo kichwa ngumu,haina maana kwamba atapatikana mbadala atakaekuwa mzuri kwa jumuiya ya NATO.
Hakuna upinzani wenye nguvu nchini Uturuki.Mpinzani wake mkubwa,ni mtu mwenye malengo yasiyojulikana. Erdogan ni mwanasiasa alienasa ndani ya shimo na kadri anavyojaribu kujinasua ndivyo nguvu zinavyozidi kumwishia.
Mwandishi: Güngör Baha
Tafsiri:Mtullya Abdu
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman