1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Kitisho cha kuliyumbisha taifa la Kenya

Josephat Nyiro Charo26 Septemba 2013

Zaidi ya watu 60 wameuwawa na wengine wengi kujeruhiwa. Umwagaji damu Nairobi umelifanya kundi la Al Shabaab kuangaziwa tena. Shambulizi la kigaidi linatishia kuiyumbisha Kenya. Lazima kupatikane suluhisho la kisiasa.

https://p.dw.com/p/19mXZ
Schmidt, Andrea Multimediadirektion REGIONEN, Afrika - Kisuaheli DW2_8365. Foto DW/Per Henriksen 18.10.2012
Deutsche Welle Afrika Kisuaheli Andrea SchmidtPicha: DW

Kwa kutumia shambulizi dhidi ya jengo lenye maduka la Westgate linalopendwa na raia wa kigeni, wataalamu na Wakenya katika eneo la Westlands jijini Nairobi, wanamgambo wa Al Shabaab walitaka kusababisha uharibifu, kuumiza hisia na kuugutusha ulimwengu kwamba wapo na wanataka wazungumziwe, anasema Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Wellef, Andrea Schmidt.

Jengo la Westgate linamilikiwa kwa sehemu na Muisraeli, na wafanyakazi katika jengo la Umoja wa Mataifa lililo karibu hupendelea kwenda kununua vitu katika duka hilo. Ndio maana kuna haja ya kupatikana sulushisho la kimataifa. Ulimwengu haupaswi kukaa kimya na kutazama yanayoendelea, kuruhusu wanamgambo wenye itikadi kali barani Afrika, sio tu nchini Kenya bali hata Nigeria ambako wanamgambo wa kundi la Boko Haram wanaendesha shughuli zao za ugaidi, waendelee kuvuruga usalama na kuyumbisha uthabiti.

Kundi la Al Shabaab, wapiganaji wa vita vya Jihadi kutoka Somalia, wenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda, wanafanya unyama na ukatili wa hali juu kabisa nchini Kenya. Kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter wamekiri kuhusika na hujuma ya jijini Nairobi na kutangaza litafanya mashambulizi mengine. Sababu waliyoitoa ni hatua ya Kenya kutuma wanajeshi nchini Somalia chini ya mwavuli wa kikosi maalumu cha kulinda amani nchini humo cha Umoja wa Afrika, AMISOM, Kikosi hicho kinachowajumuisha wanajeshi kutoka Uganda, Burundi na Kenya, kilifaulu kusaidia kuwatimua wapiganaji wa Al Shabaab na kuyakomboa na kuyadhibiti maeneo waliyokuwa wakiyadhibiti. Na hiyo pia ndio sababu kwa nini Al Shabaab imepeleka vita vyake katika taifa jirani la Kenya.

Suluhisho la kisiasa latakikana

Shambulizi hili la kinyama halitakiwi kuleta shinikizo litakalosababisha wanajeshi wa Afrika walioko Somalia waondoke nchini humo. Mpaka mpana wa Kenya na Somalia ni vigumu mno kuusimamia. Maelfu ya watu wa asili ya kisomali wanaishi nchini Kenya, taifa ambalo limekuwa kitovu cha mapambano dhidi ya wanamgambo wa al Shabaab na ambayo mara kadhaa imekabiliwa na mashambulizi ya kigaidi. Ili kuilinda nchi hiyo inayotegemea sana mapato kutokana na utalii, wanajeshi wa Kenya walitumwa Somalia mnamo mwaka 2011 kuwasaidia wanajeshi wa Umoja wa Mataifa walioko Somalia.

Kwa Wasomali ambao wamekuwa wakiteseka kwa miongo kadhaa, ni muhimu kwamba kundi la al Shabaab linachakazwa na kuangamizwa kabisa. Jumuiya ya kimataifa haipaswi kukaa ikishika tama bila kufanya chochote huku ikilitazama likiivuta nchi jirani katika vita vyake. Hatua zitakazochukuliwa na kikosi cha AMISOM zinatakiwa kuchukua mwelekeo wa kutafuta suluhisho la kisiasa. Kwa mantiki hiyo viongozi wenye msimamo wa kadri ndani ya kundi la al Shabaab wanatakiwa kuhimizwa wakae kwenye meza ya mazungumzo na wajadiliane juu ya mpango mpana kuhusu Somalia. Ni kwa njia hiyo pekee ambapo amani ya kudumu inaweza kupatikana katika taifa hilo, ambalo linawaathiri majirani zake.

Mwandishi: Schmidt, Andrea/Josephat Charo

Mhariri: Yusuf Saumu