Maoni: Mugabe anaondoka, mfumo wake wa utawala unabaki
16 Novemba 2017Pengine sababu inayowazuia wanajeshi waliochukua udhibiti wa Zimbabwe kukiri wazi kwamba wamefanya mapinduzi, ni hofu kuwa umma unaweza kuwageuka ikiwa Rais Mugabe atafanyiwa vitendo vya ukatili. Kinadharia Mugabe mwenye umri wa miaka 93 bado ni rais wa nchi, lakini mtu atakuwa rais wa namna gani, akiwa yuko katika kifungo cha nyumbani, na hana mamlaka ya kuchukua uamuzi wowote? Hana nguvu yoyote, anachoweza tu sasa ni kujadiliana kuhusu hatima ya familia yake, kisha atie saini waraka wa kujiuzulu. Yaliyobaki ni mjadala kwa wataalamu wa sheria ya katiba.
Baada ya miaka 37 madarakani, enzi ya Mugabe imefika kikomo, na mapinduzi ya kweli yamekuwa kusimamisha mchakato ambao umekuwa ukiendelea, wa kumweka mkewe Grace mwenye umri wa miaka 52 katika nafasi ya kurithi kiti cha urais.
Yote sasa ni kumhusu mwanamke huyo, sio mmewe mkongwe ambaye amedhoofika kimwili na kiakili. Waliokuwa wakimuona siku za hivi karibuni wanafahamu fika kwamba Mugabe hakuwa tena na nguvu. Grace, mkewe wa pili ambaye hapo awali alikuwa karani wake, alikuwa akilitumia jina la Mugabe kwa maslahi yake kisiasa, na kwa muda mrefu hakuna aliyethubutu kupinga. Wakosoaji walifukuzwa kutoka nafasi za madaraka. Mugabe hakufanya chochote kuizuia hali hiyo, bali aliweka imani yake yote nyuma ya mke wake.
Alipoibuka Emmerson Mnangagwa katika wadhifa wa Makamu rais, Grace hatimaye alimpata mpinzani wa kweli. Mnangagwa ni mshirika wa muda mrefu wa Rais Robert Mugabe. Amepigana katika vita vya ukombozi na amekuwa pia waziri wa ulinzi. Kwa hayo hawezi kulinganishwa na mtu mwenye taaluma ya ukarani, ambaye alikuwa na miaka 14 wakati Zimbabwe ilipopata uhuru wake mwaka 1980.
Grace Mugabe ni miongoni mwa watu wanaochukiwa zaidi nchini Zimbabwe. Sambamba na kujikusanyia utajiri mkubwa na mamlaka, amejitengezea maadui wengi kupitia kauli zake zenye ukali mithili ya sumu. Wafuasi wake wengi ni wasio wasio na chembe ya uadilifu, ambao haja yao ni kujitajirisha tu, pamoja na wakomunisti sugu. Inavyodhihirika sasa, wote wamecheza vibaya karata zao.
Kwa hali hii, jeshi ndilo chaguo bora, hususan kwa sababu hakuna chaguo mbadala. Jeshi la Zimbabwe linayo sifa ya nidhamu, na kushiriki katika mapambano dhidi ya Malaria na kipindupindu. Sifa za jeshi polisi ni kinyume kabisa na hizo za jeshi.
Zimbabwe ni nchi inayoongozwa kijeshi. Makamanda wa zamani ndio wakuu wa taasisi za serikali, na makampuni makubwa ya uchimbaji madini huingiza mapato yao moja kwa moja katika akaunti za jeshi. Wapiganaji wa zamani wako kila mahali, wengi wao, kama mwanajeshi wa kikosi cha anga Perence Shiri, wana mikono iliyojaa damu, kutokana na mauaji ya halaiki dhidi ya watu wa kabila dogo la Ndebele mnamo miaka ya 1980.
Wanajeshi waliochukua udhibiti wa nchi wanaahidi kitu kimoja tu; nacho ni utulivu. Hata mpinzani Tendai Biti aliyewahi kuwa waziri wa fedha, amelisifu jeshi kwa mpangilio ulioliwezesha kuchukua madaraka bila umwagaji damu wa raia. Lakini hakuna anayepaswa kujidanganya kwamba mapinduzi haya yatakuwa na tija yoyote kwa Zimbabwe, kwani Emmerson Mnangagwa ambaye anaweza kuongoza serikali ya mpito, ana mizizi katika mfumo uliopitwa na muda, kama alivyo Mugabe.
Mwandishi: Claus Stäcker
Tafsiri: Daniel Gakuba
Mhariri: mohammed Abdul-rahman