Maoni wa Wahariri juu ya Muhammed Mursi
10 Julai 2012Juu ya Misri, mhariri wa gazeti la "Franfkurter Allgemeine" anatilia maanani kwamba siku chache baada ya kula kiapo cha kuutumikia wadhifa wa Urais, Rais mpya wa Misri Muhammed Mursi amediriki kuchukua hatua ili kuirejesha nguzo muhimu ya demokrasia - yaani Bunge. Kwa kuchukua hatua hiyo Mursi anatumai kuungwa mkono na rafiki zake wa kisiasa na wote ambao hawamo katika kambi ya udugu wa kiislamu.
Mhariri wa gazeti la "Frankfurter Allgemeine" anasema hatua ya Mursi ni ya ujasiri katika juhudi za kupambana na majenerali. Lakini mhariri huyo anatilia maanani kwamba tayari zinatolewa kauli za kumpinga rais huyo. Watu wa Misri wanayafanya mambo yawe magumu katika njia ya kuyafanikisha mapinduzi.
Gazeti la "Südwest Presse" pia linazungumzia juu ya mvutano uliopo baina ya Rais mpya na majenerali. Linasema hakuna anayeweza kusema kwa uhakika iwapo sheria zitakazopitishwa na bunge, lililorejeshwa na Rais Mursi zitakuwa na uhalali. Na wala hakuna anayeweza kusema iwapo mahakama yatakuwa na maana tena nchini Misri.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle anafanya ziara nchini Misri, Jee ziara hiyo ina maana gani? Gazeti la "Del-men-horster Kreisblatt" linaeleza: Waziri Westerwelle anatarajiwa kukutana na Rais Mpya wa Misri wakati ambapo Misri imetingwa na mgogoro unaotokana na mvutano baina ya Rais na majenerali. Mkutano wa Westerwelle na Rais Mursi unaweza kuwakasirisha baadhi ya watu wa Misri. WaMisri na hasa vijana walioshiriki katika harakati za kuleta demokrasia nchini wanapaswa kushuhudia mvutano uliopo baina na waislamu wenye itikadi kali na baraza la majenerali ambao hasa ndiyo wanaoitawala Misri.
Gazeti la "Die Welt" linazungumzia juu ya mabadiliko katika mtazamo wa Urusi kuhusu mgogoro wa Syria. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa mambo sasa yanabadilika kwa Rais Assad. Siyo kwa sababu Syria sasa imo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Bali Urusi inapaswa kuutathimini upya mtazamo wake juu ya Syria. Pia Rais Putin aliweza kuitathimini hali ya Syria, vingine wakati wa zaira yake ya hivi karibuni nchini Israel. Kwa nini Urusi iisaidie Iran idumishe nguvu zake? Leo Iran imesimama dhidi ya Marekani, lakini huenda kesho ikasimama dhidi ya Urusi?
Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Josephat Charo