Maoni: Wasaa wa kuamua hatima ya Ulaya
23 Juni 2016Ulaya nzima inaangalia: ikitumai kuwa kura ya maoni ya Uingereza kuhusu mustakabali wake katika Umoja wa Ulaya inakamilika bila hitilafu na kuwa Waingereza watasalia katika umoja huo.
Ulaya nzima? Bila shaka hapana. Wapinzani, wanaoupinga umoja huo na maadui wa klabu hiyo wanatumai kuwa upande wa “wanaotaka kuondoka” utashinda. Iwapo Uingereza itatalikiana na Ulaya, bila shaka, kutakuwa na athari kubwa: kwa serikali zinazoupinga umoja huo, lakini hasa kwa vyama vinavyoupinga umoja wa Ulaya kama vile National Front cha Ufaransa na Freedom Party cha Uholanzi.
Katika hali hii, mtu lazima akumbuke: katika nchi hizi – ambazo zote ni wanachama waanzilishi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya, EEC – kura za maoni zilitumiwa kuipinga rasimu ya kwanza ya Katiba ya Umoja wa Ulaya. Na kuna uwezekano kuwa vyama hivyo huenda vikajaribu kutumia kura za maoni katika nchi zao kulazimisha suala la uwanachama wa Umoja wa Ulaya. Matokeo yake yanaweza kuwa ya moja kwa moja.
Mageuzi yanahitajika haraka katika Umoja wa Ulaya
Hivyo: sehemu kubwa ya Ulaya inatumai. Hasa Ulaya yenye nia timamu. Walakini, sehemu hii ya Ulaya inafahamu: hata kama Uingereza itaendelea kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, mageuzi yanahitajika kwa kiwango kikubwa. Iwapo Uingereza itabaki, umoja huo utastahili kuanza kukusanya mawazo yake kuhusu namna hali kubwa ya kutoaminiana inavyoweza kutatuliwa. Nia na madhumuni ya Ulaya lazima iwekwe wazi kwa mara nyingine tena.
Zipo hoja nyingi za msingi na kiuchumi za kwa nini Uingereza inastahili kubakia katika Umoja wa Ulaya. Na zipo hoja nyingi za msingi na kiuchumi za kwa nini Umoja wa Ulaya unastahili kuwa na Uingereza kama mwanachama. Bila ya kila mmoja, sio Uingereza wala Umoja wa Ulaya atakayeweza kutekeleza jukumu kubwa katika jukwaa la siasa za kimataifa.
Kama Uingereza itaondoka, Ujerumani itampotesha mshirika wake muhimu wakati linakuja suala la kuuona Umoja wa Ulaya kuwa zaidi ya mashine tu ya kusambaza fedha.
Upumbavu wa kisiasa
Bila kuangalia yatakavyokuwa matokeo ya kura hiyo ya maoni – kitu kimoja tayari kiko wazi. Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron aliomba na akaamua kuitisha kura hii hatari ya maoni hasa kwa sababu za kindani chamani; ambazo ni kuwanyamazisha wahafidhina wanaopinga Umoja wa Ulaya.
Kwa kufanya hivyo, ameutumbukiza Umoja wa Ulaya katika mgogoro usiojulikana hatima yake. Kinaya ni kuwa, pia ameziita pepo hizo zinazopinga ulaya ambazo alitaka zimwondokee. Ameiweka hatima ya nchi yake katika na ile ya Umoja wa Ulaya katika kura ya maoni isiyokuwa na maana yoyote. Na hataka kama Uingereza itapiga kura katika njia ambayo watu wengi wanatumai itafanya: Cameron amesababisha mgawanyiko katika nchi yake mwenyewe. Pia ameuweka Umoja wa Ulaya katika kitisho cha kusambaratika. Kwa sababu hiyo pekee, uamuzi wa kuandaa kura ya maoni ilikuwa tu ni upumbavu wa kisiasa. Na matukio ya huzuni ya wiki kadhaa zilizopita – ambapo kilele chake kilikuwa mauaji ya mbunge wa Labour nchini Uingereza Jo Cox – yamedhihirisha ukweli kuwa masuala mazito kama hayo yanapaswa kutatuliwa na wabunge na sio kura za maoni.
Mwandishi: Alexander Kudascheff/Bruce Amani
Mhariri: Yusra Buwayhid