1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Watoto wapendwa, maandalizi huleta tija

27 Septemba 2016

Kujiandaa vyema, uzoefu na kujiamini vimemsaidia Hillary Clinton wa Democratic kushinda mdahalo wa kwanza dhidi ya Donald Trump wa Republican kuelekea uchaguzi wa rais wa Novemba, Marekani. Ni maoni ya Ines Pohl wa DW.

https://p.dw.com/p/2QdDs
USA Wahlkampf TV Duell
Picha: Reuters/A. Latif

Tangu mwanzoni maswali yalikuwa je, Trump ataweza kuwa na nidhamu, je atajizuia kuwatukana wageni, wanawake au waislamu kwa kipindi chote cha dakika 90 za mdahalo? Hayo yalikuwa maswali yanayozunguka katika vyombo vya habari vya Marekani, kuhusu mdahalo wa kwanza kwa njia ya televisheni kati ya wagombea wakuu wawili, Hillary Clinton na Donald Trump.

Usijali ukweli wa kusikitisha, kwamba mjadala huu wa kuwania ofisi muhimu zaidi duniani, umeshuka hadhi kiwango hiki. Lakini hayo ndiyo maswali katika kampeni za uchaguzi huu, ambapo mazungumzo hayajikiti juu ya hoja za kisiasa na mikakati, badala yake yanazungumzia ukubwa wa mkono wa mtu na mambo mengine yaliyovuka mpaka.

Kauli zisizo na mashiko

Ines Pohl, Mwandishi wa DW
Ines Pohl, Mwandishi wa DWPicha: DW

Naam, ameweza kuwa na nidhamu, hakutoa matusi wala kashfa kwa wanawake na waislamu. Lakini hayo hayajamsaidia sana. Kinyume chake, jioni ya jana imetudhihirishia kuwa mafanikio aliyoyapata Trump mnamo miezi ya hivi karibuni mabomu ya moshi yatokayo mdomoni mwake, yametufanya kutouangazia ujinga wake.

Vile vile amefanikiwa kwa sababu vyombo vya Marekani vilikurupukia ujanja wote alioutumia katika kuvuta wafuasi, maoni ya watu kumhusu na fedha.

Ni wazi kwamba washauri wake wameamua kuhusu mabadiliko kihaiba katika kipindi hiki muhimu cha mbio za urais. Bila shaka ni katika kuwavutia wanachama wa kawaida wa Republican ambao anawahitaji sana, na ambao hadi sasa wamekataa kumuunga mkono fidhuli kama Trump. Mkakati wake huo pia umeshindwa.

Ufidhuli wake waanikwa hadharani

Mbele ya hadhara inayokadiriwa kufika watu milioni 100, Hillary Clinton amemuanika kweupe mpinzani wake. Kwa kutumia kejeli, akili na ucheshi, ameonyesha kwamba ukiacha maneno matupu na matusi ya nguoni, Trump hana jipya na hana lolote. Akikabiliwa na maswali kuhusu siasa za nje, kitisho cha ugaidi na masuala ya usalama, hata kuhusu masuala ya uchumi na kodi, Trump hakuwa na jibu zaidi ya kauli za kujisifu zilizojaa utata, ambazo kusema kweli ni dhana zilizo tupu.

Kwa yeyote aliyeutazama mdahalo huu bila kuegemea upande, Trump ameshindwa. Na sio kwa kiwango kidogo, bali kwa kishindo, kishindo kile kile ambacho kimejaa katika ahadi za kampeni yake. Kwa upande mwingine Hillary Clinton amedhihirisha juhudi kubwa anazozifanya kuandaa kazi iliyo mbele yake, na namna anavyoiheshimu ofisi ya rais.

Katika dunia ambapo raia huamua mgombea wao kwa kutumia vigezo na hoja za kisiasa, mdahalo huu unaeleza bila kuacha mashaka yoyote kwamba Donald Trump hafai kuwa mrithi wa Rais Barack Obama.

Mwangwi wa misimamo yao yenyewe

Lakini je, hayo yanaihusu jamii ambayo, kutokana na mitandao ya kijamii iliyojengwa, watu wanaishi katika dunia ndogo zilizo mkabala, ambapo watu katika dunia moja hawasikii chochote zaidi ya mwangwi wa misimamo yao wenyewe? Je mdahalo huu utaweza kujipenyeza katika dunia hizo ndogo? Bado ni mapema kumfuta Trump. Itakuwapo mijadala mingine ambayo Clinton anaweza kufanya makosa, yatakayoisaidia mitandao ile kuja juu.

Lakini leo, ni dhahiri kuwa yeye nimshindi wa mdahalo huu. Trump ameyumba. Wanasiasa ambao hawana kingine cha kutambia zaidi ya mafanikio yao, hufifia wanapozimiwa taa. Na hicho ndicho alichofanya Hillary Clinton Jumatatu usiku, akijawa na tabasamu.

Mwandishi: Ines Pohl

Tafsiri: Daniel Gakuba

Mhariri:Yusuf Saumu