Maoni ya wahariri juu ya uchumi wa Ulaya
6 Mei 2014Mhariri wa gezeti la "Der neue Tag" anasema taarifa zinazotoka kwenye nchi zinazokabiliwa na mgogoro wa kiuchumi zinazidi kutia moyo.Mhariri huyo anatilia maanani kwamba Ureno sasa imekuwa nchi ya tatu kuondoka kwenye orodha ya nchi zinazohitaji kusaidiwa. Mhariri huyo anasema hiyo ni hatua ya mafanikio.
Hata hivyo mhariri wa gazeti la "Der neue Tag" ametahadharisha kwamba bado zipo nchi zinazohitaji kusaidiwa na pia pana mashaka makubwa kutokana na mgogoro wa Ukraine.
Gazeti la "Badische" pia linazifurahia habari juu ya hali nzuri ya kiuchumi katika nchi za Ukanda wa sarafu ya Euro. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba ni hatua ya mafanikio kwa Ireland,Ugiriki na Ureno sasa kuweza kupatiwa mikopo kwa riba nafuu .Lakini anasema hizo ni nchi ndogo kiuchumi kulinganisha na Ufaransa na Italia.
Utabiri uliotolewa mwanzoni mwa mwaka umeonyesha kwamba hali bado ni mbaya nchini Ufaransa. Deni la Italia linavuka asilimia 130 ya pato jumla. Deni la Ufaransa pia ni kubwa na idadi ya watu wasiokuwa na ajira inaongezeka. Kwa kuyazingatia hayo,tunaweza kusema kwamba inapasa kuipima vizuri furaha inayojitokeza juu ya hali ya uchumi katika nchi za Ukanda wa sarafu ya Euro.
Njia bado ni ndefu
Mhariri wa gazeti la "Rhein" anaitumia kauli ya uwazi kueleza kwamba njia bado ni ndefu ya kufika mahala ambapo mtu anaweza kusema kwamba mgogoro wa madeni umeshapita. Mhariri huyo anasema hali siyo mbaya, lakini vile vile, siyo nzuri sana.
Marekani na Umoja wa Ulaya
Gazeti la "Westfälische Nachrichten" linatoa maoni juu ya mkataba wa biashara huru baina ya Umoja wa Ulaya na Marekani. Na linasema mazungumzo juu ya mkataba wa biashara huru kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani yamefanyika katika hali ya kiza kiza .
Na hiyo ndiyo sababu yamezua wasi wasi miongoni mwa watu wa Ulaya juu ya uwezekano wa viwango vya kiulaya kupuuzwa. Sasa inabidi kufanya juhudi ili kuirejesha imani ya watu hao. Hata hivyo kiwango cha madhara yaliyosababishwa na wajumbe kwenye mazungumzo, kitabainika baada ya kufanyika uchaguzi wa Bunge la Ulaya.
Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen.
Mhariri: Yusuf Saumu