1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yalaumiwa juu ya Syria

13 Oktoba 2015

Wahariri wa magazeti leo wanatoa maoni juu ya mgogoro wa Syria na juu ya uhusiano baina ya Uturuki na Umoja huo.Pia wanazungumzia juu ya ziara ya Kansela Merkel nchini Uturuki.

https://p.dw.com/p/1GnBy
Rais wa Syria Bashar al-Assad na wanajeshi wake
Rais wa Syria Bashar al-Assad na wanajeshi wakePicha: picture-alliance/AP Photo

Gazeti la "Nordwest" linasema wanasiasa wa Umoja wa Ulaya hawajaielewa asili ya utawala wa Al- Assad .Utawala huo ni wa kikatili lakini bado unaungwa mkono na idadi kubwa ya wananchi wa Syria.

Urusi haijafungua njia za kidiplomasia nchini Syria

Gazeti la "Badische" linatoa maoni juu ya kujiingiza kijeshi kwa Urusi katika mgogoro wa Syria.

Mhariri wa gazeti hilo anasema hatua zinazochukuliwa na Urusi kwa ajili ya kumpa nguvu Rais Assad, hazijafungua njia mpya za kidiplomasia. Ni silaha tu zinazosikika. Mhariri huyo anaeleza kwamba jawabu la Marekani ni kusimama pamoja na mfungamano wa kidemokrasia wa watu wa Syria na kuongeza msaada wa silaha.

Gazeti la "Badische" linatilia maanani kwamba kwa wanajihadi Syria ni uwanja wa vita vya jihadi. Kutokana na hali hiyo dhamira ya kuvimaliza vita vya nchini Syria haiko kabisa.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" linazungumzia juu ya uhusiano baina ya Umoja wa Ulaya na Uturuki katika muktadha wa mgogoro mkubwa wa wakimbizi. Mhariri wa gazeti hilo anasema nchi za Umoja wa Ulaya zitaweza kuidhibiti mipaka iwapo tu nchi jirani zitachangia katika juhudi hizo.

Mhariri wa gazeti la "Der Tagesspiegel" anatilia maanani kwamba katika suala hilo Uturuki inahusika zaidi kuliko nchi nyingine .

Mhariri huyo anaeleza kuwa, Umoja wa Ulaya utaweza kukataa kuwachukua wakimbizi,wanaotaka kuingia katika nchi za Umoja huo, ikiwa utaitangaza Uturuki kuwa kituo cha kwanza ambapo wakimbizi waliingia na ambapo wanapaswa kusajiliwa.

Bila ya kufikia mapatano na Uturuki maalfu ya wakimbizi wataendelea kumiminikia katika nchi za Umoja wa Ulaya. Mhariri wa gazeti la "Der Tagesspiegel" anasema Umoja wa Ulaya hauna budi ushirikiane na Uturuki na pia uwe tayari kutoa nyenzo kwa Uturuki zitakazoiwezesha nchi hiyo kuwashughulikia wakimbizi watakaokuwa wanarudi katika nchi hiyo baada ya kukatiliwa katika nchi za Umoja wa Ulaya.

Kansela Merkel kufanya ziara Uturuki

Gazeti la "Landeszeitung " linatoa maoni juu ya ziara ambayo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anatarajia kufanya nchini Uturuki Jumapili ijayo. Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba Kansela Merkel anafanya ziara hiyo wakati ambapo Uturuki imo katika pilika pilika za kampeni za uchaguzi.Na pia anafanya ziara hiyo licha ya mihemko iliyojitokeza baada ya shambulio la kigaidi.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: imago/IPON

Kansela Angela Merkel amesema Uturuki imara ni jambo la manufaa kwa Ujerumani vile vile, linatilia maanani gazeti la "Landszeitung."

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa ni jambo la kusikitisha kuwa Ujerumani imechelewa kuutambua ukweli huo.Na kutokana na maslahi yake ya kibinafsi Ujerumani inataka kulizuia wimbi la wakimbizi kwa msaada wa Uturuki.

Lakini gazeti la "Landeszeitung" linasema Kansela Merkel anakwenda katika nchi iliyogawanyika na ambayo haiwezi kuimarishwa na Umoja wa Ulaya.

Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman