1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsipras autibua Umoja wa Ulaya

Admin.WagnerD8 Aprili 2015

Wahariri wa magazeti leo wanatoa maoni juu ya ziara ya Waziri Mkuu wa Ugiriki nchini Urusi na juu ya hali mbaya sana katika kambi ya wakimbizi wa Yarmuk nchini Syria.

https://p.dw.com/p/1F46H
Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras afanya ziara Urusi
Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras afanya ziara UrusiPicha: Reuters/I. Sekretarev

Juu ya ziara ya Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras nchini Urusi gazeti la "Volksstimme"linasema bila shaka Tsipras atalakiwa kwa moyo mkunjufu na mwenyeji wake Rais Vladimir Putin.

Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba Waziri Mkuu Tsipras anafanya ziara hiyo wakati ambapo pana mvutano baina ya Urusi na nchi za magharibi mithili ya vita baridi katika miaka ya nyuma.

Mhariri huyo anakumbusha kwamba wakati huo pia viongozi wa nchi za magharibi walikuwa wanakwenda Urusi. Lakini hatari iliyopo sasa ni kwamba Ugiriki inaweza kuwa tegemezi kwa Urusi.

Tsipras anafanya makosa

Mhariri wa gazeti la "Der Tagesspiegel" anasema Waziri Mkuu wa Ugiriki anakosea sana, kwa kufanya ziara nchini Urusi. Mhariri huyo anafafanua kwamba wengi katika Umoja wa Ulaya walikuwa tayari kuifungua mifuko yao kwa ajili ya Ugiriki laiti serikali ya nchi hiyo ingelionesha kwamba nayo ipo tayari kuutoa mchango wake. Waziri Mkuu Tsipras inapita katika njia potovu.

Ugiriki bado inao marafiki katika Umoja wa Ulaya ambao wapo tayari kuisaidia ,lakini siyo Urusi. Ni bora kwa Tsipras kwenda makao makuu ya Umoja wa Ulaya mara 20 . Washirika wake watamsuburi.


Gazeti la "Thüringische Landeszeitung" linasema anachofanya Waziri Mkuu wa Ugiriki ni kichekesho. Kwani hawezi kuutisha Umoja wa Ulaya, Ujerumani wala Marekani. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza katika maoni yake kuwa kelele za Ugiriki kudai fidia za madhara yaliyosababishwa na Ujerumani ya Hitler wakati wa vita kuu vya pili ambapo Ugiriki ilikaliwa na mafashisti, ni njama nyingine za Ugiriki.

Madai ya Ugiriki hayawezi kutimizwa

Mhariri wa gazeti hilo anaishauri serikali ya Ujerumani inapaswa iwe na msimamo thabiti lakini wa utulivu na kusubiri mashtaka ya Ugiriki. Anasema hakuna anaekanusha kuhusika kwa Ujerumani katika madhara yaliyotokea nchini Ugiriki wakati wa vita kuu vya pili. Lakini madai ya Ugiriki ya kulipwa fidia ya Euro Bilioni 278 hayawezi kutimizwa katika msingi wa sheria za kimataifa.

Hali yazidi kuwa mbaya katika kambi ya Yarmuk
Gazeti la "Kölner Stadt-Anzeiger" linasema hali inazidi kuwa mbaya katika kambi ya wakimbizi ya Yarmuk nchini Syria. Gazeti hilo linaeleza kwamba kinachotokea katika kambi hiyo ni mfano wa yale yanayotokea nchini Syria kote.

Watu wametenganishwa kabisa na huduma muhimu .Watu wa Syria sasa hawajui wakiogope kitu gani zaidi : njaa,mabomu yanayodondoshwa na ndege za Assad au wawaogope wale wanaoitwa Dola la Kiislamu wanaoishambulia kambi hiyo yenye wakimbizi 18,000

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Iddi Ssessanga