1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

jaribio lililoshindikana

Admin.WagnerD9 Aprili 2015

Wahariri wa magazeti leo wanatoa maoni juu ya ziara ya Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras nchini Urusi na pia wanauzungumzia mgogoro wa Yemen

https://p.dw.com/p/1F5YI
Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras na Rais wa Urusi Vladimir Putin
Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras na Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: picture-alliance/dpa/Zemlianichenko

Juu ya ziara ya Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras nchini Urusi gazeti la "Mittelbayerische" linasema Rais Vladimir Putin anajaribu kuzivutia upande wake nchi ndogo ndogo za Umoja wa Ulaya.

Mhariri huyo anasema ,madhali Umoja wa Ulaya una wanachama 28 na jumla ya watu Milioni 450, ziara ya Tsipras nchini Urusi ni sawa na kujaribu kumuua tembo kwa ubua. Hatahivyo, anaeleza mhariri huyo, Umoja wa Ulaya hauwezi kunyamaza kimya ikiwa kila mwanachama atajaribu kuifuata sera yake binafsi ya mambo ya nje.

Tsipras aiuza Ulaya

Mhariri wa gazeti la "Bild" ametumia maneno makali katika kuikosoa ziara ya Waziri Mkuu wa Ugiriki Tsipras nchini Urusi kwa kusema Alexis Tsipras ni Waziri Mkuu wa nchi mojawapo ya Umoja wa Ulaya lakini yeye si mwana Ulaya.

Mhariri huyo anasena aliyoyafanya na aliyoyasema jana mjini Moscow yanaliharakisha jambo moja tu: kusambaratika kwa nchi yake na hivyo kuupa kisogo Umoja wa Ulaya. Tsipras inaielekeza nchi yake ,Ugiriki, nje ya Ulaya!Anawauza watu wake pamoja na hazina zote za Ulaya.

Sera za kubana matumizi yailemea Ugiriki

Gazeti la "Sächsiche" linasema kimsingi Umoja wa Ulaya una haki ya kuionya Ugiriki dhidi ya kutoka nje ya mstari wa Umoja huo na kuitaka nchi hiyo iifuate sera y pamoja. Lakini mhariri wa gazeti hilo anasema viranja wa jumuiya hiyo wanalisahau jambo moja muhimu na anaeleza kuwa sera ya kubana matumizi ya Umoja wa Ulaya inayoibana Ugiriki ndiyo iliyomfanya Waziri Mkuu wa nchi hiyo atafute msaada kutoka mbali.Na ukweli ni kwamba Umoja wa Ulaya hauna zaidi cha kutoa kwa Ugiriki.

Viranja hao wa mrengo wa kihafidhina katika Umoja wa Ulaya pia wanasahau kwamba waliyafumbia macho yaliyotendwa na serikali za kihafidhina za hapo awali nchini Ugiriki.

Vita vya Yemen vinazidi kuwa vikubwa

Mhariri wa gazeti la "Volksstimme" anauzungumzia mgogoro wa nchini Yemen katika muktadha wa makubaliano yaliyofikiwa mjini Lausanne baina ya Iran na mataifa sita muhimu. Mhariri huyo anasema bado watu wanakumbuka jinsi watu nchini Iran walivyosherehekea makubaliano ya mjini Lausanne baina ya nchi yao na mataifa sita muhimu. Lakini mhariri anasema furaha hiyo inaweza kutoweka haraka.

Kutokana na kushtadi kwa mgogoro wa Yemen,mvutano baina ya Iran na Saudi Arabia unazidi kuwa mkubwa. Vita vya kiwakala nchini Yemen, baina ya Iran na Saudi Arabia vinaweza kusababisha moto mkubwa katika eneo lote la ghuba.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Iddi Ssessanga