1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Abdu Said Mtullya31 Oktoba 2012

Wahariri watoa maoni juu ya ziara ya Waziri Mkuu wa Uturuki nchini Ujerumani na juu ya mgombea Ukansela wa Ujerumani wa chama cha SPD Steinbrück na pia wanauzungumzia uvumi juu ya Ufaransa kufilisika

https://p.dw.com/p/16Zwr
Mgombea Ukansela wa chama cha SPD Peer Steinbrüeck. ,
Mgombea Ukansela wa chama cha SPD Peer Steinbrück.Picha: AFP/Getty Images

Waziri Mkuu wa Uturuki Erdogan anafanya ziara nchini Ujerumani. Mhariri wa gazeti la Neue Presse anatilia maanani kwamba Uturuki inaathirika na vita vya nchini Syria na hasa kutokana na kupokea idadi kubwa ya wakimbizi. Mhariri wa" Neue Presse" anasema msaada wa Ujerumani unahitajika, siyo tu, kwa sababu za kibinadamu , bali pia kwa sababu ya kuiunga mkono Uturuki.

Katika maoni yake Gazeti la "Bild linauliza jee ni kweli, Ufaransa ipo njiani kuifuata Ugiriki katika matatizo ya bajeti? Mhariri wa gazeti hilo amemnukuu aliekuwa Kansela wa Ujerumani Gerhard Schröder akisema kuwa Ufaransa inaweza kuwa Ugiriki nyingine katika Ukanda wa sarafu ya Euro. Mhariri huyo anasema; Jee inawezekana kwa taifa kubwa la Ufaransa kuwa muflisi kama Ugiriki. Hapana bado. Lakini Ufaransa imekalia tawi linalonesanesa.

Nchi hiyo bado ina mfumo wa kazi wa saa 35 kwa wiki na pia inakabiliwa na matatizo ya kimiundo kama yale ya Ujerumani miaka 10 iliopita. Kama mwanzilishi mmojawapo wa Umoja wa Ulaya Ufaransa inao wajibu wa kuilinda sarafu ya Euro. Na kwa hivyo sasa Rais Hollande lazima achukue hatua za kuleta mageuzi.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine "linakizungumzia Kimbunga Sandy, kwa kutilia maanani kampeni za uchaguzi wa Rais nchini Marekani. Mhariri wa gazeti hilo anasema, pamoja na pilika pilika zote za kampeni,mfumo wa kuyashughulikia majanga ya asili lazima ufanye kazi nchini.

Jee mwanasiasa anaechuma fedha nyingi anaweza kuwa kiongozi mwafaka wa kutetea maslahi ya watu wadogo katika jamii?. Hilo ni swali la mhariri wa gazeti la "Neue Osnabrücker" juu ya mgombea Ukansela wa Ujerumani,Peer Steinbrück.
Mwanasiasa huyo wa chama cha SPD yupo chini ya shinikizo kwa sababu ya malipo makubwa aliyoyapata kutokana na mihadhara aliyoitoa.

Mhariri wa "Neue Osnabrücker anatoa maoni yake kwa kusema kwamba Steinbrück amechukua hatua inayostahili. Amepiga kifua na kujitokeza mbele na kutoa maelezo yote. Sasa ni juu ya wale wanaomsakama kutoka vyama vya CDU na FDP kujua ni hatua gani nyingine ya kuichukua. Hata hivyo mhariri anasema bado pana swali la kuuliza juu ya mwanasiasa huyo mahiri wa kutoa hoja. Ndiyo ameeleza kila kitu kwa uwazi, lakini jee yeye kama mwanasiasa anaepata fedha za pembeni,hadi kufikia zaidi ya Euro Milioni moja anaweza kuyaelewa matatizo ya watu wadogo ?

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu