Mkutano muhimu kwa Kansela Merkel
16 Februari 2016Gazeti la "Badische Tagblatt "linasema mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya utakaofanyika mwishoni mwa wiki hii utakuwa muhimu hususan kwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.
Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba , ikiwa viongozi wa Umoja wa Ulaya hawatakubaliana juu ya suluhisho la pamoja,uzito wa Kansela Merkel utapwaya.
Mhariri huyo pia anakumbusha kwamba fedha ambazo Uturuki iliahidiwa bado hazijakusanywa na mipango ya dharura kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi haifanyi kazi kwa ufanisi. Na kwa hivyo huenda viongozi wa Umoja wa Ulaya wakajaribu kutafuta njia za kuurefusha muda tu.
Gazeti la "Der neue Tag" pia linasema mambo yamekaa kombo kwa Kansela Merkel .Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba Kansela Merkel anatamani kuuona Umoja wa Ulaya ukizumgumza kwa sauti moja juu ya mgogoro wa wakimbizi. Lakini matamanio hayo sasa hayana msingi kwa sababu pamezuka kundi la nchi nne linaloitwa , " Visegrad "linalotofautiana naye.
Naye mhariri wa gazeti la "Flensburger Tageblatt" anauzungumzia mkutano wa jana wa mawaziri wakuu wa nchi hizo nne - Poland,Hungary,Jamhuri ya Czech na Slovakia.
Mhariri huyo anakumbusha kwamba hapo awali Kansela Merkel alikuwa mwanasiasa maarufu miongoni mwa nchi hizo za Ulaya ya kati. Lakini tangu Kansela huyo, aonyeshe ukarimu mkubwa kwa wakimbizi , na tangu atoe pendekezo juu ya kugawana wakimbizi hao kwa njia ya haki, nchi hizo nne, sasa zimegeuka kuwa mahasimu wa kiongozi huyo wa Ujerumani.
Ni maoni ya nchi hizo zinazoitwa "Visegrad" kwamba sera ya Ujerumani juu ya wakimbizi si sahihi.
Mpango wa Uturuki kupeleka majeshi Syria ni hatari
Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaitahadharisha Uturuki juu ya mpango wake wa kupeleka majeshi nchini Syria. Mhariri wa gazeti hilo anasema mpango huo ni wa hatari! Anaeleza kwamba wakati wote Uturuki inakuja na vitendawili. Sasa inafikiria juu ya kupeleka majeshi nchini Syria. Mpango huo utaifanya hali iwe ya kutatanisha zaidi nchini Syria.
Wakurdi wanaozingatiwa kuwa washirika wa Marekani, katika kupambana na magaidi wa dola la kiislamu , ni magaidi kwa Uturuki. Gazeti la Hannoversche, linaiambia Uturuki wazi kwamba majeshi yake nchini Syria yanaweza kuvaana na yale ya Urusi, na kwa hivyo isitumai kuona mshikamano wa nchi nyingine za NATO.
Mwandishi:Mtullya abdu,Deutsche Zeitungen.
Mhariri:Yusuf Saumu