1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

181009 Buchmesse Abschluss

Josephat Nyiro Charo19 Oktoba 2009

Idadi ya wageni yapungua mwaka huu

https://p.dw.com/p/KAK9
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alipoyafungua maonyesho ya Frankfurt Oktoba 13Picha: AP

Maonyesho ya vitabu ya mwaka huu mjini Frankfurt hapa Ujerumani yamemalizika jana. Idadi ya watu waliohudhuria maonyesho hayo ambayo China ilikuwa mgeni wa heshima, ilipungua kidogo, lakini hata hivyo yamebakia kuwa maonyesho makubwa yanayoongoza duniani kwa waandishi na wachapishaji wa vitabu na mawakala. Kulikuwa na zaidi ya vibanda 7,000 kutoka nchi mbalimbali duniani na vitabu vipya 123,000 vilionyeshwa kwenye maonyesho hayo.

Jumla ya wageni 290,469 walihudhuria maonyesho ya mwaka huu ya vitabu mjini Frankfurt yaliyomalizika hapo jana. Idadi ya watu waliojitokeza kwenye maonyesho hayo ilipungua kwa asilimia 2.9 ikilinganishwa na mwaka jana 2008 wakati maonyesho hayo yalipofanyika kwa mwaka wa 60. Meneja wa mradi wa maonyesho ya vitabu ya Frankfurt, bwana Peter Ripken, amesema kupungua kwa wageni mwaka huu kumesababishwa na mgogoro wa kiuchumi.

Mwishoni mwa maonyesho hayo ya Frankfurt hapo jana tuzo ya amani ya vitabu inayotolewa na wachapishaji vitabu wa Ujerumani, ilitunukiwa Claudio Magris katika kanisa la Paulskirche mjini Frankfurt. Magris mwenye umri wa miaka 70 ni mwandishi wa vitabu na msomi kutoka Italia ambaye pia huchangia makala kwenye gazeti akijikita katika maswala kuhusu Ulaya ya Kati.

Katika hotuba yake ya kuikubali tuzo hiyo aliyotunukiwa, yenye thamani ya euro 25,000, Magris alionya juu ya ubabe wa kisiasa barani Ulaya na kukosoa vizuizi visivyoonekana kati ya wahamiaji na wazawa katika miji mikubwa ya Ulaya.

"Leo hii kuna mipaka mingine inayotishia amani. Mipaka isiyoonekana katika miji yetu kati yetu na wageni wanaokuja kutoka sehemu zote za ulimwengu ambayo hatuizingatii. Wakimbizi huwasili kila mara katika pwani ya Italia ambao huchukuliwa kuwa maharamia. Jinsi wanavyoshughulikiwa inatatiza na ni dalili za ukatili."

Claudio Magris Frankfurter Buchmesse 2009
Claudio MagrisPicha: picture-alliance / Sven Simon

Claudio Magris ameshinda zawadi nyingi za Ulaya na ametajwa kuwa miongoni mwa watu wanaopigiwa upatu kushinda tuzo ya amani ya Nobel ya uandishi sanifu.

Maonyesho ya vitabu ya Frankfurt mwaka huu yalizusha utata kwa kuwa China ilikuwa mgeni wa heshima. Mjadala mkubwa ulizuka kuhusu haki za binadamu. Mkurugenzi wa maonyesho ya vitabu ya Frankfurt Jürgen Boos amedokeza mwishoni mwa maonyesho hayo kuwa ameridhika kwamba China ilikuwa mgeni wa heshima mwaka huu. Mkurugenzi huyo aidha amesema ilikuwa muhimu kuialika China kwani imewezekana kuyaangazia maswala mengi ya nchi hiyo na kuanzisha majadiliano.

Pia ujumbe rasmi wa China umetoa tathimini nzuri juu ya maonyesho ya vitabu ya mjini Frankfurt na unajivunia kwamba wageni wengi walipendelea kuvitembelea vibanda 600 vya China kwenye maonyesho hayo.

Akitoa tathimni yake kuhusu maonyesho ya vitabu ya Frankfurt mwandishi wa vitabu na mtaalam wa maswala ya China, bwana Tilman Spengler amesema, "Kwanza nilikuwa na hisia kwamba kutokana na hali hii ya mvutano tungekuwa na mijadala kuhusu siasa, jamii, haki za binadamu na kadhalika. Lakini hayo hayakujitokeza. Kuna mambo mengi kuhusu China yaliyowasilishwa na kujadiliwa mambo mapya yaliyomo kwenye bidhaa za China. Kwa njia hiyo China imefahamika zaidi na watu wameilewa zaidi. Hilo ni jambo zuri."

Argentina itakuwa mgeni wa heshima katika maonyesho ya vitabu ya Frankfurt ya mwaka ujao 2010 yaliyopangwa kufanyika kauanzia Oktoba 6 hadi Oktoba 10.

Mwandishi : Rabitz Cornelia/ZR/Josephat Charo

Mhariri:M.Abdul-Rahman