Mapatano kati ya Israel na Hamas yaingia siku ya mwisho
27 Novemba 2023Makubaliano ya kusitisha vita kati ya Israel na kundi la Hamas yameingia siku yake ya nne na ya mwisho leo Jumatatu huku wanamgambo hao wakisema wako tayari kurefusha utekelezaji wa makubaliano hayo baada ya kuwaachia huru mateka zaidi.
Miongoni mwa mateka 17 zaidi walioachiwa na Hamas, jana ni pamoja na mtoto yatima mwenye umri wa miaka 4 ambaye wazazi wake walikuwa miongoni mwa watu waliouwawa katika uvamizi wa Oktoba 7 uliofanywa na Hamas dhidi ya Israel.
Soma pia: Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Hamas na Israel yanamaliza muda wake Jumatatu
Wapatanishi wa kimataifa akiwemo mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Joseph Borrell wanashinikiza usitishwaji mapigano uendelezwe.
Rais wa Marekani Joe Biden amesema anataraji makubaliano hayo ya muda mfupi yanaweza kuendelezwa mradi mateka wanaendelea kuachiwa huru.
Kundi la Hamas limesema ikiwa juhudi zitafanyika za kuwaachia Wapalestina zaidi walioko kwenye jela za Israel watakuwa tayari kuendelea kusitisha vita.