1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Mapigano mapya yautikisa mji mkuu wa Khartoum

27 Septemba 2024

Mapigano mapya yanayojumuisha mashambulizi ya angani kutumia droni na ndege za kivita yameutikisa ndani na viunga vya mji wa Khartoum nchini Sudan kuanzia jana Alhamisi.

https://p.dw.com/p/4l9VZ
Moshi ukifuka mji mkuu wa Khartoum
Moshi ukifuka mji mkuu wa KhartoumPicha: AFP

Jeshi la Sudan lilianzisha operesheni mapema Alhamisi, kwa lengo la kuchukua udhibiti wa baadhi ya maeneo ya mji huo mkuu wa Sudan, ambayo yamekuwa mikononi mwa wanamgambo wa RSF, ambao ni maadui wake.

Vyombo vya habari vya Sudan vimeripoti kuhusu ongezeko la hatua za kijeshi ikiwemo mashambulizi makubwa ya angani kuwahi shuhudiwa katika miezi ya hivi karibuni katika wilaya za Khartoum na Omdurman.

Soma: UN yazitaka pande hasimu Sudan kusitisha mapigano wakati wa Ramadhan

Kupitia taarifa, msemaji wa wizara ya Afya Mohammed Ibrahim amesema raia wanne waliuawa na wengine 14 walijeruhiwa kwenye wimbi hilo jipya la mashambulizi katika wilaya ya Omdurman, mji ulioko mkabala na Khartoum.

Mwanaume mmoja akikagua athari za mashambulizi mjini Khartoum
Mwanaume mmoja akikagua athari za mashambulizi mjini KhartoumPicha: AFP

Msemaji wa jeshi alithibitisha kuwa operesheni hiyo inaendelea, lakini alisita kutoa maelezo zaidi.

Mkuu wa jeshi la Taifa Jenerali Abdel-Fattah Burhanalilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York ambapo alisema « tumefanya kila kitu chini ya uwezo wetu, ili kusitisha vita hivyo na kuitoa nchi yetu kwenye uharibifu unaoendelezwa na wanamgambo ».

Alikariri msimamo huo huo´alipozungumza na waandishi wa habari Alhamisi jioni na kusema « Operesheni inayoendelea Khartoum inakusudia kuhifadhi uadilifu wa nchi yetu, usalama wa watu wetu na walinda usalama wetu. »

vikosi," Aliongeza kuwa hatua za kijeshi ni suluhu la mwisho, na kwamba wanatamani kuwepo suluhisho la amani linalowazuia wananchi kukumbwa na mateso, njaa na kulazimika kuyahama makwao.

Soma: Miripuko ya mabomu imerindima tena mjini Khartoum

Burhan aliyeongoza mapinduzi ya mwaka 2021 nchini humo, ni mshirika wa karibu wa taifa jirani Misri na rais wa nchi hiyo ambaye pia ni mkuu wa zamani wa majeshi Abdel Fattah el-Sissi.

Ufafanuzi: Je ni nchi zipi zinahusishwa na vita vya Sudan?

Sudan ilitumbukia kwenye mgogoro mnamo Aprili, 2023 kufuatia mvutano wa muda mrefu kati ya jeshi linaloongozwa na Burhan na wanamgambo wa RSF wanaoongozwa na Mohammed Hamdan Dagalo, na kugeuka kuwa vita kamili katika mji mkuu Khartoum.

Tangu wakati huo, mapigano yameenea katika maeneo mengine ya nchi hsa maeneo ya mijini na kaskazini mwa Darfur.

Juhudi za upatanishi na kusitisha mapigano ambazo zimekuwa zikiongozwa na Saudi Arabia, Marekani na washirika wengine hazijafua dafu.Mashambulizi yarindima Sudan, mazungumzo ya amani yakiendelea

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield amesema zaidi ya watu milioni 25 nchini SUdan wanakabiliwa na kitisho kikubwa cha njaa na kwamba takriban watu milioni 11 wamelazimika kuyakimbia makaazi yao. Greenfiel alitaja mgogoro wa SUdan kuwa mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu ulimwenguni na ni sharti pande zote husika zishinikizwe kukubali usitishaji vita kuwezesha shughuli za kiutu.