Mapigano yachacha Ukanda wa Gaza wanajeshi watatu wa Israeli wauwawa
6 Januari 2009Mapigano makali yanaripotiwa kuendelea leo jumanne mashariki ya mji wa Gaza kati ya Hamas na vikosi vya Israeli.vikosi vya Israeli vimezungumza mji wa Gaza City.Ndege za kijeshi za Israel zimerusha mabomu kwenye jengo la ofisi za usalama la Hamas katikati ya mji wa Gaza na kuliacha likiwaka moto lakini hakuna mtu aliyeko ndani ya jumba hilo.Aidha Kwa upande mwingine kundi la Hamas linaendelea kurusha roketi ndani ya Israel linasema limerusha makombora dhidi ya vifaru sabaa vya wanajeshi wa Israeli kwenye eneo la Dhejaiya na kuwaua wanajeshi 10 lakini vituo vya televisheni vya kiarabu vya Aljazeera na Al arabiya ambayvo vina waandishi wake ndani ya Gaza vinasema kwamba wanajeshi wa Isreali waliouwawa ni watatu au wanne na wengine 30 wamejeruhiwa.Lakini jeshi la Israeli limesema wanajeshi wake watatu ndio waliouwawa baada ya kufyatuliwa risasi kwa bahati mbaya na wenzao waliokuwa katika kifaru.
Vile Vile Juhudi za kidiploamisia zinaendelea rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa ameitolea mwito Israeli kusimamisha vita lakini mwito huo umepingwa vikali na waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert ambaye amesema makubaliano yoyote ya kusitisha vita ambayo hayatakomesha uvurumishaji wa roketi kutoka kundi la Hamas dhidi ya Israeli hayawezi kukubalika.Sarkozy alikutana na Olmert baada ya kuwa na mazungumzo na rais wa mamlaka ya wapalestina Mahmoud Abbas na rais Hosni Mubarak wa Misri aliyesimamia makubaliano ya amani ya miezi sita yaliyomalizika muda wake desemba 19 na kufuatiwa na mzozo wa sasa.Rais Sarkozy amesema Umoja wa Ulaya unataka kuwepo makubaliano ya amani haraka iwezekanavyo.
Aidha Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon amewataka viongozi wanaohusika kuchukua hatua za dharura na kuumaliza haraka mzozo huo wa Gaza unaosababisha umwagikaji mkubwa wa Damu.Amesema baraza la usalama linabidi kuzingatia jukumu lake.
Baraza la usalama la Umoja wa mataifa linatazamiwa kuwa na mkutano wa ngazi ya mawaziri hii leo kujadiliana juu ya mwito uliotolewa na nchi za kiarabu wa kutaka usitishwaji haraka wa vita na pia kulindwa raia wa palestina.Kwa upande mwingine ujumbe wa Umoja wa Ulaya pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Misri walikuwa na mkutano mjini Cairo na kuzungumzia juu ya kulitaka baraza la usalama la Umoja huo wa mataifa kupitisha azimio la kukomesha mapigano.Wakati huohuo Marekani bado imekataa kuizuia Israeli ikomeshe vita dhidi ya Gaza.