1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano Yemen yatishia mpango wa amani Hodeidah

15 Desemba 2018

Siku moja baada pekee baaday a pande zinazozozana kukubaliana kuweka chini silaha, mapigano yamezuka karibu na mji wa Hodeidah.

https://p.dw.com/p/3AAYF
Jemen Huthi-Loyalist in Sanaa
Picha: picture-alliance/dpa/XinHua/Mohammed

Mapigano yalizuka Ijumaa jioni kati ya wapiganaji wanaoiunga mkono serikali na waasi wa Houthi karibu na mji muhimu wa bandari wa Hodeida, ikiwa ni ya kwanza ya aina yake tangu pande zinazozozana zilipokubaliana kusitisha mapigano siku moja kabla.

Wakaazi walisema walisikia milio ya risasi katika viunga vya mashariki mwa Hodeidah, wakati televisheni ya Wahouthi ya al-Masirah ikiripoti kuwa ndege za kivita za muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia zilifanya mashambulizi kaskazini mwa mji huo.

Siku ya Alhamisi, wawakilishi wa serikali ya Yemen na wajumbe wa Houthi waliunga mkono makubaliano ya kuweka chini silaha ndani na nje ya mji wa Hodeida, ambao ndilo lango kuu la kupitisha misaada ya kiutu na chakula kwa nchi hiyo inayokabiliwa na baa la njaa.

Waangalizi wanahitajika

Lakini mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo wa Yemen Martin Griffiths ameonya jana kuwa bila waangalizi nchini humo, mpango wa kusitisha mapigano huenda ukasambaratika haraka sana.

"kikosi thabiti cha waangalizi sio tu muhimu; pia kinahitajika haraka mno,” Griffiths aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano, pande zinazozana zilisema zitayaondoa majeshi yao na kuyapeleka "katika maeneo nje ya mji na bandari zake.” Kwa Umoja wa Mataifa udharura huo hauwezi kupuuzwa.

Adam Baron kutoka Baraza la Ulaya kuhusu Mahusiano ya Kigeni ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa "mchakato uliotangazwa kuhusu Hodeidah unakabiliwa na uwezekano wa kuvunjika – muhimu itakuwa ni kuhakikisha mchakato wenye mpangilio wa kuondoka wapiganaji na kuwazuia wasumbufu kuuvuruga mchakato huo,”

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Zainab Aziz