Marekani itafanya mazungumzo na Assad kuvimaliza vita
16 Machi 2015Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema Marekani haina budi kufanya mazungumzo na Rais wa Syria Bashar al Assad ili kutafuta njia za kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimeingia mwaka wake wa tano hapo jana.
Kerry amesema wamekuwa wakitaka kufanya mazungumzo na utawala wa Syria kwa misingi ya makubaliano ya kutafuta amani ya Geneva.
Hata hivyo msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Marie Harf amesema hakuna mabadiliko katika sera ya Marekani kuhusu mzozo wa Syria na mazungumzo yoyote iwapo yatakuwepo yatakuwa ni baina ya Marekani na wawakilishi wa Assad na sio ya moja kwa moja na kiongozi huyo.
Syria imetelekezwa na jumuiya ya kimataifa
Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, zaidi ya watu laki mbili wameuawa na takriban nusu ya idadi ya raia wa Syria wameachwa bila ya makaazi katika mzozo ambao makundi ya kutetea haki za binadamu yameishutumu jumuiya ya kimataifa kwa kuitelekeza Syria.
Mzozo huo wa Syria ambao ulianza na maandamano ya kumtaka Rais Assad kuondoka madarakani, umechukua mikondo tofauti, wanajeshi wa serikali wakipambana na waasi wanaomtaka Assad kuondoka madarakani, huku wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi linalojiita dola la kiislamu kwa upande mwingine wakipambana na wapiganaji wa kikurdi.
Akihojiwa na kituo cha televisheni cha CBS hapo jana Kerry amesema shinikizo zaidi linahitajika ili kuishurutisha serikali ya Assad kurejea katika meza ya mazungumzo baada ya duru mbili za mazungumzo kukwama mjini Geneva.
Waziri huyo wa Marekani mapema mwezi huu alikutana na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov kujadili namna ya kuyaanzisha tena mazungumzo hayo ya kutafuta amani Syria.
Urusi ambayo ni mshirika mkubwa wa Assad inaendesha mchakato kivyake kuutafutia ufumbuzi mzozo huo wa Syria na itakuwa mwenyeji wa mazungumzo yanayotarajiwa mwezi ujao ambayo haijabainika iwapo upande wa upinzani nchini Syria utahudhuria mazungumzo hayo ya Moscow.
Kufuatia matamshi ya Kerry kuwa huenda Marekani hatimaye ikalazimika kuzungumza na Assad, Uingereza imetoa tamko ikisema Assad hana nafasi katika mustakabali wa Syria na kuongeza nchi hiyo itaendelea kuiwekea Syria vikwazo hadi utawala wa Assad utathmini upya msimamo wake, uvimalize vita na ukubali kufanya mazungumzo ya tija na upande wa upinzani.
Mzozo wa Syria mkubwa zaidi katika enzi ya sasa
Shirika la kutetea haki za binadamu la Syria limesema kiasi ya watu 215,518 wameuawa tangu mzozo huo kuanza huku thuluthi moja kati ya hao wakiwa raia wakiwemo zaidi ya watoto elfu kumi.
Idadi kamili ya waliouawa inakisiwa kuwa kubwa kuliko hiyo kwa sababu hatima ya maelfu ya watu ambao hawajulikani waliko haijulikani. Shirika la kushughulikia maslahi ya wakimbizi la umoja wa Mataifa UNHCR limesema mzozo wa Syria ndiyo janga kubwa la kibinadamu katika enzi ya sasa.
Kiasi ya wasyria milioni nne wamekimbilia nchi jirani za Lebanon, Jordan na Uturuki na kuzitwisha nchi hizo mzigo mkubwa wa kukidhia mahitaji yao.
Nchini Syria kwenyewe zaidi ya watu milioni saba wameachwa bila ya makaazi na umoja wa Mataifa umesema takriban asilimia sitini ya watu wa Syria ni maskini.
Kinyume na ilivyokuwa mwanzoni mwa vita vya Syria, nchi za magharibi hivi sasa zinaonekana kulegeza kamba dhidi ya kumtaka Assad kung'olewa madarakani na kutiwa wasiwasi na kitisho cha kuibuka kwa makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali kama la dola la kiislamu.
Mwandishi:Caro Robi/Afp/Reuters
Mhariri: Gakuba Daniel