Marekani kuishinikiza Myanmar kufuata njia ya demokrasia
6 Septemba 2023Makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris amesema hii leo katika mkutano na viongozi wa mataifa ya jumuiya ya ASEAN, kwamba taifa lake litaendelea kuishinikiza Myanmar kufuata njia ya demokrasia.
Amesema, ASEAN imeonyesha mafanikio katika kushughulikia mapinduzi ya Myanmar na mengineyo ya kikanda na kuongeza kuwa ushirika huo kwa kiasi kikubwa unasalia kuwa jukwaa lenye umuhimu, ambapo pia ametangaza kuanzishwa kwa kituo kipya cha ushirikiano kati ya Marekani na ASEAN, mjini Washington.Mkutano wa jumuiya ya ASEAN waanza Jakarta
"Sisi kama Wamarekani tunaamini tuna maslahi mapana katika suala la usalama wetu, lakini pia ustawi wa sasa na wa wakati ujao katika kuendeleza na kuimarisha mahusiano kwa namna mbalimbali, kupitia diplomasia ambayo kwa sehemu inanifanya niendelee kuzuru ukanda huu, lakini pia kile tunachotakiwa kufanya ili kuendeleza uhusiano kupitia ustawi na manufaa ya pande zote".
Harris anayehudhuria mkutano huo kwa niaba ya rais Joe Biden aidha amewasifu viongozi wa ASEAN kwa kujitoa kwao katika kufuata kanuni za kimataifa na kushughulikia masuala ya kikanda.