1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuondoa wanajeshi wake 12,000 kutoka Ujerumani

Saleh Mwanamilongo
30 Julai 2020

Jumla ni wanajeshi 11,900 wa Marekani ambao wataondolewa nchini Ujerumani.Na watakaosalia ni wanajeshi 24.000 kutoka jumla ya wanajeshi 36,000

https://p.dw.com/p/3gBu1
Tangazo la awali la rais Trump la kuondoa wanajeshi wake lilishangaza jumuiya na NATO na serikali ya Ujerumani.
Tangazo la awali la rais Trump la kuondoa wanajeshi wake lilishangaza jumuiya na NATO na serikali ya Ujerumani.Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Waziri wa ulinzi wa Marekani Mark Esper ameainisha mpango wa kuwarejesha nchini Marekani, wanajeshi wapatao 6,400 kutoka Ujerumani, na kuwahamishia wengine 5,400 katika mataifa ya Ulaya. Mpango huo ikiwa utatekelezwa, utapunguza uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini Ujerumani kwa karibu theluthi moja.

Jumla ni wanajeshi 11,900 wa Marekani ambao wataondolewa nchini Ujerumani. Na watakaosalia ni wanajeshi 24.000 kutoka jumla ya wanajeshi 36,000 alisema waziri wa ulinzi wa Marekani Mark Esper.

Mwezi uliopita, rais wa Marekani Donald Trump aliidhinisha kuondolewa kwa zaidi ya robo ya wanajeshi wa nchi yake walioko Ujerumani, akisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha usalama barani Ulaya.Serikali ya Trump iliitaka Ujerumani kuongeza mchango wake kwenye bajeti ya ulinzi ili kufikia lengo la mchango wake kwenye jumuiya hiyo ya NATO la asilimia 2 ya pato lake jumla la ndani.

Esper  amewaambia  waandishi  habari kuwa karibu wanajeshi 5,600 watahamishiwa katika  mataifa  mengine ya  jumuiya  ya  NATO, wakati 6,400 watarejea  nchini Marekani, ambapo  wengi  watabadilishwa  kutoka  sehemu moja  kwenda nyingine  katika  bara  la  Ulaya.

''Bado ni mwanzo wa taratibu hiyo''

Ameongeza  kuwa  hatua  hiyo inafanyika, katika  hali ambayo  itaimarisha  jumuiya  ya  NATO,kuimarisha vizuwizi dhidi ya Urusi,kutoa hakikisho kwa washirika na  kuimarisha uwezo wa Marekani kuchukua  hatua za kimkakati.Esper hakufafanua kuhusu muda wa kuondolewa kwa wanajeshi hao lakini anasema kwamba operesheni hiyo itagarimu dola bilioni kadhaa.

Marekani imewafahamisha wanachama wa NATO kuhusu hatua yake.
Marekani imewafahamisha wanachama wa NATO kuhusu hatua yake.Picha: picture-alliance/AP Photo/Operation Resolute Support Headquarters/Sgt. Justin T. Updegraff

Mabadiliko mengine makubwa kuhusu uongozi na operesheni maamulu za jeshi la Marekani barani Ulaya ni kwamba makao makuu ya jeshi hilo kwa bara la Ulaya yataondolewa mjini Stuttgart (Ujermani) na kupelekwa mjini Mons,Ubeljiji alisema Tod Wolters,kamanda wa kikosi cha wanajeshi wa Marekani barani Ulaya.

Waziri wa Ulinzi wa Ubeljiji,Philippe Goffin amepongeza uamuzi wa Marekani wa kuhamisha ngome ya jeshi lake nchini humo.

''Tunazingatia pendekezo hilo la Marekani, ambalo litajadiliwa ilikufahamu ni aina gani ya wanajeshi watakao letwa hapa na ni majukumu gani watakayopewa hapa au Italia.Bado ni mwanzo wa taratibu hiyo.''

''Zawadi kwa Urusi''

Nchini Marekani hatua hiyo imepokelewa kwa maoni tofauti kwenye chama cha upinzani cha Demokratika na hata katika chama cha Republican ambapo wanahofia kudhoofishwa kwa jumuiya ya NATO dhidi ya Urusi.

Mwezi Juni,Maseneta sita walitangaza mageuzi ya sheria kuhusu ulinzi wa taifa ifikapo mwaka 2021 inayositisha matumizi ya fedha kwa ajili ya kupunguza kwa wanajeshi wa Marekani nchini Ujerumani.

Mitt Romney,moja wa maseneta hao aliitaja hatua ya utawala wa Trump kuwa ni ''kosa kubwa, aibu kwa rafiki na mshirika Ujerumani, na zawadi kwa Urusi''.

Katibu mkuu wa jumuiya ya NATO, Jens Stoltenberg alisema kwamba Marekani ilijadiliana na nchi wanachama wa NATO kabla ya kutangaza hatua hiyo ya kuondoa wanajeshi wake nchini Ujerumani.Tangazo la awali la Rais Trump liliishangaza jumiya ya NATO na serkali ya Ujerumani.