Marekani: Mapigano kusitishwa kwa saa 72 Mashariki mwa Kongo
12 Desemba 2023Katika taarifa, msemaji wa Baraza la Usalama la kitaifa la Ikulu ya White House Adrienne Watson, amesema vikosi vya kijeshi na vikundi vya wapiganaji visivyokuwa vya kiserikali viliacha kupigana ili kuruhusu kuondolewa kwa vikosi vilivyokuwa katika maeneo ya Mushaki na Barabara ya RP1030, kuanzia jana mchana. Watson ameongeza kwamba Marekani itatumia intelijensia yake na raslimali za kidiplomasia kufuatilia shughuli za vikosi vya kijeshi na makundi mengine yenye silaha yasiyo ya kiserikali wakati wa muda huo wa kusitisha mapigano.
Msemaji wa serikali ya Rwanda hakujibu mara moja ombi la tamko kuhusiana na makubaliano hayo. Msemaji wa rais wa Kongo Felix Tshisekedi pia hakutoa tamko.
Kundi la M23 lashtumiwa kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano
Wachambuzi wanasema, makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoafikiwa mwezi Novemba mwaka jana yanaripotiwa kukiukwa na kundi la M23. Hata hivyo, kundi hilo limekanusha madai hayo. Msemaji wa M23 Willy Ngoma, anasema muda huo wa kusitisha mapigano kwa masaa 72 hauhusiani na kundi hilo na kwamba muda huo ni wa kuepusha kuongezeka kwa mvutano zaidi kati ya Kongo na Rwanda.
Ngoma ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba siku zote kundi la M23 linaheshimu muda wa kusitishwa kwa mapigano.
Bintou Keita aonya kuhusu kuendelea kwa visa ya ukosefu wa usalama
Onyo la mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Kongo Bintou Keita kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, limekuja muda mfupi kabla ya mabalozi kutoka Kongo na Rwanda kutuhumiana wakati wa mkutano wa baraza hilo na siku tisa kabla ya uchaguzi wa rais nchini Kongo wa Disemba 20, ambapo Rais Felix Tshisekedi anagombea kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili.
Akilihutubia baraza hilo Keita amesema kwamba ukosefu wa usalama unaendelea katika eneo la Mashariki, hasa kuhusiana na mgogoro wa M23 uliozuka upya, lakini pia kuibuka kwa visa vipya vya ukosefu wa usalama katika maeneo mengine ya nchi, hasa eneo la Katanga pamoja na mikoa ya Mai-Ndombe na Tshopo kuwa mbaya katika eneo la Kivu Kaskazini.
Mabalozi wa Rwanda na Kongo watuhumiana wakati wa mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa
Wakati wa mkutano wa baraza hilo, balozi wa Kongo Zenon Mukongo aliwashtumu wanajeshi wa Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 na kutaja matukio kutoka mwezi Novemba mwaka 2022.
Alisisitiza wito wa nchi yake wa kukomeshwa kwa uchokozi wa Rwanda, kuondolewa kwa vikosi vyake na kutokomezwa kwa makundi ya wapiganaji wenye silaha nchini Kongo yanayolijumuisha kundi la M23, huku akilihimiza baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa kuchukuwa hatua kufanikisha haya.
Soma pia: Jeshi la Congo, askari wa UN watangaza operesheni ya pamoja dhidi ya waasi wa M23
Kwa upande wake, balozi mpya wa Rwanda katika Umoja huo wa Mataifa Ernest Rwamucyo, ameishtumu serikali ya Kongo na kile alichokiita kuwa ''muungano wake wa makundi haramu yenye silaha na mamluki wa kigeni" kwa kukiuka mchakato wa amani uliosimamiwa kikanda.