1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na India zafikia makubaliano ya nyuklia

25 Januari 2015

Rais Barack Obama wa Marekani na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi wamefanikiwa kuondowa mkwamo wa makubaliano ya nyuklia na kupongeza enzi mpya ya urafiki kati ya mataifa hayo mawili makubwa ya kidemokrasia duniani.

https://p.dw.com/p/1EQFH
Rais Barack Obama wa Marekani na Waziri Mkuu wa India Narenda Modi mjini New Delhi. (25.01.2015)
Rais Barack Obama wa Marekani na Waziri Mkuu wa India Narenda Modi mjini New Delhi. (25.01.2015)Picha: Reuters/J. Bourg

Baada ya kusalimiana na Obama kwa kumkumbatia wakati alipowasili New Delhi Jumapili(25.01.2015) kwa ndege yake ya Air Force One Modi baadae aliuchangamkia uhusiano huo mpya na kiongozi mwenzake katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu mjini New Delhi.

Obama ambaye utawala wake hadi mwaka mmoja uliopita ulikuwa ukimuona Modi kama ni mtu alietengwa na jamii amesema urafiki wao mpya unaonyesha uhusiano wa asili kati ya mataifa hayo mawili ambayo yote yanatafuta njia ya kuweka uwiano wa kuzuwiya kuongezeka kwa ushawishi wa China.

Wakati kukiwa hakuna maazimio yoyote yale makubwa yaliofikiwa mbali na kuyakwamua makubaliano ya nyuklia,Modi amesema uamuzi wa Obama kuwa rais wa kwanza wa Marekani kuitembelea India mara mbili wakati akiwa madarakani kiishara una umuhimu mkubwa sana.

Uhusiano wa kirafiki na maelewano

Modi ameuambia mkutano wa waadishi wa habari "Uhusiano baina ya nchi hautegemei sana hatua za kuusimamisha na kusitishwa bali zaidi juu ya uhusiano kati ya viongozi na hususan maelewano baina yao.

Rais Barack Obama wa Marekani akisalimia kwa mila ya Kihindu (katikati) ni Rais wa India Pranab Mukherjee (kushoto) ni Waziri Mkuu Narendra Modi .New Delhi. (25.01.2015)
Rais Barack Obama wa Marekani akisalimia kwa mila ya Kihindu (katikati) ni Rais wa India Pranab Mukherjee (kushoto) ni Waziri Mkuu Narendra Modi .New Delhi. (25.01.2015)Picha: picture-alliance/dpa/EPA/H. Tyagi

Amesema "Barack na Mimi tumeweza kuwa na urafiki madhubuti ......na maelewano hayo sio tu yametuweka karibu bali pia yamezidi kuziweka karibu serikali za nchi hizi mbili na watu wake."

Baada ya kuanza kutamka kwa Hindi maneno mawili matatu,Obama pia ameupongeza uhusiano binafsi na kiongozi mwenzake kwa kusema kwamba ukaribu wao unaonyesha kujitolea kwao kwa pamoja kwa maadili ya demokrasia na biashara.

Obama amesema ziada ya uhusiano binafsi pia wanaonyesha mapenzi yaliopo kati ya watu wa Marekani na India.

Mazungumzo ya masaa matatu

Viongozi hao wamekuwa na mazungumzo ya zaidi ya masaa matatu na kuonyesha kufikia mafanikio makubwa ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili kufuatia mzozo wa mwishoni mwa mwaka 2013 ambao ulishuhudia bendera ya Marekani ikitiwa moto katika mitaa ya Delhi.

Rais Barack Obama akiweka shada la mauwa kwenye kumbukumbu ya Mahatma Ghandhi.New Delhi.(25.01.2015)
Rais Barack Obama akiweka shada la mauwa kwenye kumbukumbu ya Mahatma Ghandhi.New Delhi.(25.01.2015)Picha: Reuters/Stringer

Kuchaguliwa kwa Modi hapo mwezi wa Mei kuliiumisha kichwa serikali ya Marekani ambayo ilikuwa imemuweka kwenye orodha ya watu wabaya mwanasiasa huyo wa siasa za Uzalendo wa Kihindu kwa zaidi ya muongo mmoja baada ya ghasia za umwagaji damu za kijamii katika jimbo la Gujarat wakati yeye alipokuwa waziri kiongozi wa jimbo hilo.

Alirudishwa tena katika mawasiliano mwezi wa Februari mwaka jana wakati balozi wa Marekani wakati huo Nancy Powell alipokwenda Gujarat mara ilipojulikana kwamba Modi yumkini akauagusha katika uchaguzi utawala wa miaka 10 wa chama che mrego wa wastani kushoto cha Congress.

Tokea aingie madarakani hakuonyesha kinyongo chochote kile na alimwalika binafsi Obama awe rais wa kwanza wa Marekani kuwa mgeni wa heshima katika gwaride la siku ya Jamhuri ya India hapo Jumatatu.

Makaribisho makubwa

Obama alipokewa kwa mzinga 21 na gwaride rasmi lililoandaliwa kwa heshima yake.Ameweka shada la mauwa kwenye kumbukumbu ya Mahatma Ghandhi ambaye ni shujaa wa taifa hilo.

Yeye na mkewe Michelle walikuwa watembelee kasri la Taj Mahal lakini safari yake hiyo imefupishwa ili kumuwezesha kwenda Saudi Arabia kutowa heshima zake kwa Mflame mpya Salman.

Rais Barack Obama wa Marekani na mkewe Michelle Obama baada ya kuwasili New Deldi katikati ni Waziri Mkuu wa India Narendra Modi. (25.01.2015)
Rais Barack Obama wa Marekani na mkewe Michelle Obama baada ya kuwasili New Deldi katikati ni Waziri Mkuu wa India Narendra Modi. (25.01.2015)Picha: picture-alliance/AP Photo

Habari ziligonga vichwa vya habari katika ziara yake hiyo ni kuhusu mkataba wa nyuklia ambapo ulikuwa umecheleweshwa mara kadhaa tokea usainiwe hapo mwaka 2008.Mkataba huo ulikuwa uiwezeshe India kupata teknolojia ya nyuklia kwa matumizi ya kiraia lakini ulikwamishwa kutokana na wasi wasi wa Marekani kuhusiana na sheria kali za India juu ya nani wa kubeba dhamana wakati inapotokea ajali ya nyuklia.

Modi amesema amefarajika kwamba miaka sita baada ya kusaini makubaliano hayo baina ya nchi mbili sasa watakuwa wanaelekea kwenye ushirikiano wa kibiashara kwa kuzingatia sheria za India na wajibu wa kimataifa.

Wakati hakuna ufafanuzi uliopatikana mara moja juu ya jinsi mkwamo huo ulivyondolewa imeripotiwa kwamba India imeanzisha bima za kuzifidia kampumi ambazo zitajenga mitambo hiyo ya kuzalisha umeme kwa nguvu za nyuklia.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/Reuters

Mhariri : Mohammed Khelef