Marekani na wengine wapinga ushindi wa Maduro Venezuela
24 Agosti 2024Washington, ambayo imeweka vikwazo dhidi ya utawala wa Maduro, imesema kupitia msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje Vedant Patel kuwa uamuzi huo hauna uhalali. Uhispania na Mexico zimeendelea kusisitiza kuhusu kutolewa kwa ripoti pana ya matokeo ya kura zilizopigwa. Mahakama ya Juu, inayozingatiwa pakubwa kuwa tiifu kwa Maduro, iliridhia ushindi wake tata wa kuongoza kwa muhula wa tatu wa miaka sita. Maduro ameuita kuwa wa kihistoria.
Upinzani inasema matokeo ya vituo vya kupigia kura yanaonesha kuwa mgombea wao Edmundo Gonzalez Urrutia, mwanadiplomasia mstaafu mwenye umri wa miaka 74, alimshinda Maduro kwa kura nyingi. Mwanasheria Mkuu Tarek William Saab, anayeonekana kuwa mshirika wa Maduro, amesema amemuita Gonzalez Urrutia ili aeleze kuhusu jukumu lake la kuchapisha matokeo baada ya uchaguzi huo.