1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Undumilakuwili wa polisi

8 Januari 2021

Idara ya polisi ya Marekani imekosolewa kwa jinsi ilivyoshughulikia uvamizi katika majengo ya bunge mjini Washington. Huo ni undumilakuwili wa polisi anaandika Carla Bleiker. 

https://p.dw.com/p/3ngJq
USA Proteste und Ausschreitungen in Washington
Picha: Jim Urquhart/REUTERS

Polisi ilionekana kuwa na kasi kubwa ya kukabiliana na maandamano ya kupinga visa vya ubaguzi wa rangi mwaka uliopita, hata hivyo ilionekana kuingiwa "baridi" kuwakabili watu waliovamia majengo ya bunge kwa sababu wengi walikuwa wazungu.

Wafuasi wa Donald Trump mjini Washington hawakufanikiwa katika jaribio lao la kupindua matokeo ya uchaguzi. Mapema jana Alhamisi, wawakilishi wa baraza la Marekani na bunge la seneti walithibitisha ushindi wa Joe Biden na Kamala Harris na kuwafungulia njia ya kuingia Ikulu.

Hata hivyo, kilichotokea kabla ya hapo kitasalia kuwa doa katika historia ya Marekani.

Wakihimizwa na Rais Donald Trump, wafuasi wake waliwashinda nguvu polisi katika majengo ya bunge na kuingia ndani ya Jumba la Capitol. Wafuasi hao walinyanyua bendera na kupiga picha wakiwa ndani ya bunge na pia kuiba vitu kadhaa vya spika Nancy Pelosi.

Soma zaidi: Polisi aliyekabiliana na waandamanaji Marekani, afariki

Katika sokomoko hilo ndani majengo ya bunge, watu wanne walipoteza maisha yao akiwemo mwanamke mmoja aliyepigwa risasi.

Mkuu wa idara ya polisi mjini Washington Robert Contee katika mkutano na waandishi habari alisema watu 52 wamekamatwa, huku wengi wao wakitiwa hatiani kwa makosa ya kukiuka agizo la kutotoka nje baada ya saa kumi na mbili jioni.

Matukio hayo ya majengo ya bunge yameibuka maswali mengi hata kuliko majibu. Watu wanajiuliza kwa nini polisi walionekana kuwa watulivu kuwakabili wafuasi wa Trump tofauti na jinsi walivyokuwa wakiwakabili waandamanaji waliokuwa wanapinga vitendo vya ukatili wa polisi kwa watu weusi.

Maandamano ya Black Lives Matter yalikabiliwa vikali na polisi

Bild des Jahres 2020 I England I Patrick Hutchinson I Waterloo station
Picha: Dylan Martinez/REUTERS

Punde tu baada ya mauaji ya Mmarekani mweusi George Floyd aliyeuawa na polisi mzungu, maelfu ya waandamanaji walikusanyika katika miji mbalimbali nchini Marekani kulalamikia visa vya ubaguzi na ukatili wa polisi dhidi ya watu weusi. Maandamano hayo yalipewa jina la Black Lives Matter.

Mnamo Juni 1, 2020 vikosi vya usalama vilivyokuwa vimejihami vilitumia nguvu kupita kiasi ikiwemo gesi ya kutoa machozi kuwakabili waandamanaji.

Soma zaidi: Marekani: Miito yaongezeka ya kumwondoa Trump madarakani mapema

Vugu vugu la Black Lives Matter liliandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, maandamano yao yalikabiliwa kwa nguvu kubwa na kasi ya ajabu ilhali wazungu wanapojaribu kufanya mapinduzi ya serikali, polisi inaonekana baridi.

Melvin Edwards, Mmarekani mweusi ambaye ni mwandishi wa vitabu mjini Maryland amesema hakushangazwa na jinsi polisi ilivyokosa kuchukua hatua katika uvamizi wa Jumatano.

"Hakika, inaonekana wazi kuna tofauti ya kiwango cha nguvu ya polisi inapokabiliana na makundi tofauti ya watu. "

Ameiambia DW kuwa, polisi ina dhana kuwa kundi fulani la watu huzua vurugu zaidi kuliko watu wengine. "Nadhani kwa ujumla inachukuliwa kuwa watu weusi ni hatari kuliko wazungu."

Kocha wa timu ya mpira wa vikapu ya Philadelhia Doc Rivers anauliza: Umejiuliza ni kitu gani kingetokea iwapo watu weusi ndio wangevamia majengo ya bunge?