Ahadi hiyo imetolewa leo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dk. Donald Wright ambaye amezuru katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu inayohifadhi wakimbizi 130,000 kutoka nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Balozi Donald amebainisha kuwa mwaka huu wa fedha, Marekani ilitoa zaidi ya dola milioni 30 kwa huduma za wakimbizi na msaada nchini Tanzania na kwamba imetenga kiasi cha dola milioni 14 nyingine kwa ajili ya wakimbizi kupitia shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR na washirika wake.
Hata hivyo licha ya Marekani kuendelea kutoa fursa za ukaaji kwa wakimbizi wa DRC, kwa upande wa Warundi hali ni tofauti kutokana na msimamo wa mashirika na serikali ya Tanzania na Marekani kutotoa kipaumbele kwao kupata hifadhi katika nchi ya tatu.
Mwakilishi mkazi wa UNHCR Tanzania, Antonio Kanhandula ameiambia DW kuwa, UNHCR inaendelea kutoa huduma stahiki kwa wakimbizi wote na kwamba hifadhi ya nchi ya tatu siyo kipaumbele.
Kwa upande wao wakimbizi kutoka Kongo na Burundi wamelalamikia kuwepo kwa upungufu mkubwa wa huduma za kijamii hususani chakula, nishati ya kupikia, madawa na wahudumu wa afya hali inayowakatisha tamaa ya usalama wao.
Kwa upande wake idara ya wakimbizi ya serikali ya Tanzania, kupitia kwa Mkurugenzi wake Sudi Mwakibasi imemuomba balozi wa Marekani kushirikiana na wadau wengine kutatua changamoto hizo, hususani kuni na chakula ili kuondoa manung'uniko kwa wakimbizi.
Hii ni mara ya kwanza kwa Balozi wa Marekani Donald Wright kuuzuru mkoa wa Kigoma na kuzitembelea kambi za wakimbizi. Prosper Kwigize, DW Kigoma.