Marekani yaishutumu Syria kutumia tena silaha za kemikali
2 Februari 2018Afisa wa ngazi ya juu waa Marekani amesema inasadikika kuwa Rais Bashar al-Assad wa Syria alificha sehemu ya shehena ya silaha za kemikali licha ya makubaliano kati ya Marekani na Urusi yalioitaka serikali yake kuzisalimisha silaha hizo ili ziharibiwe mnamo mwaka 2014.
Vikosi vya jeshi la serikali ya Assad badala yake vimeimarisha ubora wa silaha zake za kemikali na kuendelea kuzitumia kwa kiwango kidogo kila baada ya muda tokea shambulio la hatari la Aprili mwaka jana lililopelekea Marekani kuishambulia kwa makombora kambi ya kijeshi ya Shayrat nchini Syria, amesema afisa huyo katika mkutano na waandishi wa habari.
Maafisa wa Kimarekani wamekariri shutuma za hivi karibuni alizozitoa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson kwamba Urusi mshirika wa karibu wa rais Assad katika vita nchini humo, anabeba lawama ya kushindwa kutimiza jukumu lake la kuhakikisha marufuku ya silaha za kemikali inatekelezwa.
"Nadhani ni wazi kwamba Urusi ina ushawishi, lakini inafanya uamuzi usiofaa. Imeamua kutotumia ushawishi ulionawo katika serikali ya Syria. Na kuiachia serikali hiyo kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake, kwa mara nyingine tena, ni jambo lisilofaa kabisa," amesema Heather Nauert, msemaji mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani katika mkutano na waandishi habari.
Urusi hata hivyo imepinga kuhusika huko, na kusema kwamba serikali ya Syria imekana kufanya mashambulizi ya kemikali.
Mapigano lazima yasitishwe Idlib
Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umeonya kwamba mapigano yanayoendelea Kaskazini-Magharibi mwa Syria yanatishia kuongeza kasi ya mgogoro wa kibinaadamu ambao tayari umeshasababisha maelfu ya watu kupoteza makaazi yao. Jan Egeland, Mshauri Maalumu wa kikosi cha misaada ya kiutu cha Umoja wa Mataifa nchini Syria , amesema hali ya jimbo la Idlib inahitaji kusitishwa mapigano.
"Hali ya huko inahitaji kusitishwa mapigano.Niliwaambia wajumbe wa kikosi cha misaada ya kibinadamu kwamba hatuwezi kuwa na vita katika eneo linalolingana na kambi ya wakimbizi. Idlib inaishi wakazi wengi na imejaa wakimbizi na watu waliopoteza makaazi yao," Jan Egeland, mshauri Maalumu wa ujumbe wa Umoja wa Maatifa nchini Syria.
Watu milioni 1.2 kati ya 2.4 wamepoteza makaazi yao katika jimbo hilo. Ikiwa inaungwa mkono na Urusi pamoja na Iran, serikali ya Syria imekuwa ikifanya mashambulizi dhidi ya Idlib kutoka Kusini na Mashariki tokea mwishoni mwa mwaka uliopita. Jimbo hilo ni moja wapo ya ngome za mwisho za waasi nchini Syria na pia ni eneo linalokaliwa na wanamgambo wengi wenye magungamano na kundi la kigaidi la al-Qaeda.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/dpae
Mhariri: Daniel Gakuba