Trump aitoa Marekani mkataba wa nyuklia wa Iran
8 Mei 2018Trump alisema mkataba huo umeoza kabisa kuanzia katika shina lake na anatumai kuafikiana makubaliano na Korea Kaskazini. Aliueleza mkataba kati ya Iran na nchi za Magharibi kuwa mbaya na unaoegemea upande mmoja.
Kauli ya Trump imekuja wakati alipotangaza mipango ya kuiondoa Marekani kutoka mkataba huo wa kihistoria na Iran wa mwaka 2015 wakati wa hotuba aliyoitoa kupitia televisheni katika ikulu ya mjini Washington. Trump alisema kama angeuruhusu mkataba huo kuendelea kuwepo, kungetokea katika siku chache zijazo mashindano ya silaza hza nyuklia. Pia alisema mkataba wa maana ungeeweza kuafikiwa wakati huo, lakini hilo halikufanyika.
Rais huyo wa Marekani ameieleza Iran kuwa "utawala wa ugaidi mkubwa". Trump amesema Wairan wanastahili serikali bora zaidi kuliko ile iliyopo madarakani. Na alisema "hakuna hatua iliyochukuliwa na utawala wa jamhuri hiyo ya kiislamu ambayo haijawa hatari zaidi kuliko kuendelea na mpango wake wa kutaka kumiliki silaha za nyuklia na njia za kuzisafirisha."
Mshauri wa Trump wa masuala ya usalama wa taifa, John Bolton, alisema uamuzi wa Marekani unatoa ujumbe mzito kwa Korea Kaskazini kwamba haitakubali mkataba mbovu usiofaa.
Trump alisema waziri wa mashauri ya nchi za nje wa Marekani, Mike Pompeo, yuko mjini Tokyo nchini Japan, akielekea Korea Kaskazini na alitarajiwa kuwasili katika kipindi cha saa moja ijayo. Ziara hiyo inafanyika kabla mkutano uliopangwa kati ya Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un. Hii ni ziara ya pili ya Pompeo Korea Kaskazini. Trump alifichua mwezi uliopita kwamba Pompeo alikutana na Kim wikendi ya Pasaka mwaka huu. Trump alisema makubaliano yameafikiwa kuhusu siku na saa ya mkutano wake na Kim lakini bado anasubiriwa kutaja ni wapi atakapokutana na kiongozi huyo wa Korea Kaskazini.
Israel yaunga mkono hatua ya Marekani
Wakati haya yakirifiwa waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alisema anamuunga mkono rais wa Marekani kwa uamuzi wake wa kijasiri kujiondoa kutoka kwa mkataba wa nyuklia na Iran, ambao kiongozi huyo wa Israel amekuwa akiukosoa mara kwa mara.
"Israel inaiunga mkono kikamilifu uamuzi wa rais Trump kuukataa mkataba wa maangamizi wa nyuklia," alisema Netanyahu katika hotuba aliyoitoa kupitia televisheni, akizungumzia mkataba kati ya mataifa ya magharibi na Iran, taifa ambalo ni hasimu mkubwa wa Israel.
Israel imewaamuru maafisa wake katika milima ya Golan kufungua na kuandaa maeneo ya kujificha kutokana na mashambulizi ya mabomu baada ya kutambua kile ambacho jeshi limekieleza kuwa ni "shughuli zisizo za kawaida za vikosi vya Iran nchini Syria". Tangazo hilo lilitolewa dakika chache kabla rais wa Marekani Donal Trump kutangaza kuiondoa nchi yake kutoka kwa mkataba wa nyuklia wa Iran wa mwaka 2015, hatua ambayo yumkini ikachochea hali ya wasiwasi katika kanda hiyo.
Kwa upande mwingine Saudi Arabia nayo pia imemuunga mkono rais Trump katika uamuzi wake. Hayo yameripotiwa na televisheni ya taifa ya Saudi Arabia. Televisheni hiyo pia imetangaza kwamba Iran ilitumia faida za kiuchumi ilizozipata baada ya kuondolewa vikwazo kuliyumbisha eneo zima la Mashariki ya Kati.
Wakati huo huo, Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zimesema bado zinauunga mkono mkataba wa Iran na zimejitolea kwa dhati kuhakikisha unatekelezwa licha ya uamzi wa rais Trump.
Mwandishi:Josephat Charo/dpae/ap