1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Marekani yakamilisha kuteketeza silaha za kemikali

8 Julai 2023

Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza kuwa nchi hiyo imeteketeza shehena ya mwisho ya silaha zake za kemikali, hatua inayosifiwa kuwa mafanikio makubwa kuelekea dhamira ya kuondoa silaha za aina hiyo kote ulimwenguni.

https://p.dw.com/p/4TcOh
Rais Joe Biden wa Marekani
Rais Joe Biden wa Marekani Picha: Patrick Semansky/AP/dpa/picture alliance

Tangazo la Biden limefuatia ukamilishaji wa kazi ya karibu miaka minne iliyokuwa ikifanywa kwenye kituo kimoja cha kijeshi huko Kentucky ya kuteketeza kiasi tani 500 za silaha za sumu ambazo ndiyo ilikuwa akiba ya mwisho ya silaha hizo nchini Marekani.

Biden amesema anaona fahari kuwa Marekani imekamilisha kazi hiyo ya kuondoa kutoka uso wa dunia shehena ya silaha zinazofahamika kuwa na uwezo wa kuangamiza idadi kubwa ya watu.

Silaha za kemikali zinazojumuisha gesi za sumu na viambata vingine hatari zilipigwa marufuku duniani chini ya mkataba wa mwaka 1993 , tangu wakati huo shirika la kimataifa la kuzuia silaha za kemikali duniani limefanya kazi ya kusimamia uteketezaji wa silaha hizo kote  ulimwenguni.