1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yakataa pendekezo la Poland kutuma ndege Ukraine

9 Machi 2022

Marekani imelikataa pendekezo la Poland la kutowa ndege za kijeshi za enzi za Kisovieti ili zikabidhiwe kwa Ukraine katika kuisaidia kwenye mapambano yake dhidi ya uvamizi wa Urusi, ikisema haliwezi kutetewa.

https://p.dw.com/p/48COf
NATO | Polnische Luftwaffe F-16
Picha: Lithuanian Ministry of National Defense/AP Photo/picture alliance

Makao makuu ya jeshi la Marekani, Pentagon, imelikataa pendekezo la kushangaza la Poland kwamba ingeliipa Marekani ndege zake za kijeshi kwa ajili ya kutumiwa na Ukraine, katika kile kinachotajwa kama ishara isiyo ya kawaida ya kutokubaliana wakati washirika wa muungano wa kijeshi wa NATO wakisaka kuwapa nguvu wanajeshi wa Ukraine bila kujihusisha moja kwa moja na uhasama na Urusi.

Msemaji wa Pentagon, John Kirby, alisema siku ya Jumatano (Machi 9) kwamba tangazo la Poland kwamba inakusudia kuwasilisha ndege zake 28 za kjeshi chama MiG-29 katika kituo cha kijeshi cha Marekani cha Ramstein nchini Ujerumani "linazusha wasiwasi mkubwa kuhusiana na ndege za kijeshi kuondoka Marekani na kwenda kituo cha NATO na kuruka kwenye anga ambalo linawaniwa na Urusi katika mzozo wake na Ukraine."

Hata hivyo, Kirby aliongeza kwamba, hata hivyo, wangeliendelea kushauriana na Poland na washirika wengine wa NATO juu ya suala hilo. Tayar, Urusi ilishatangaza kwamba kulisaidia jeshi la anga la Ukraine kutahisabiwa kama kushiriki vita na kutajibiwa kikamilifu.

Zelensky azishukuru Marekani na Uingereza

London Parlament Videobotschaft der Präsidenten Wolodymyr Selenskyj
Wabunge wa Uingereza wakimpigia makofi Rais Volodymyr Zelensky baada ya kuwahutubia kwa njia ya video siku ya Jumanne (Machi 8).Picha: empics/picture alliance

Rais Volodymyr Zelensky aliwashukuru viongozi wa Marekani na Uingereza kwa kupiga marufuku mafuta ya Urusi kuingia kwenye nchi zao. Zelensky aliita marufuku hiyo kuwa ni ishara kubwa kwa ulimwengu mzima, akisema sasa Urusi itapaswa kuheshimu sheria za kimataifa na kuacha kuanzisha vita ama ikose fedha.

Akizungumza na bunge la Uingereza, Zelensky alisema wakati alipoanza kuhutubia picha ya kuogofya zaidi ilikuwa ya watoto 50 waliouawa ndani ya siku 13 za vita, lakini wakati anamalizia walishafikia 52.

Rais huyo aliapa kutokusamehe wala kusahau maovu yaliyotendwa na wale aliowaita wavamizi na wakaliaji. Hata hivyo, Zelensky alitumia hotuba yake kutowa tena wito wa majadiliano ya kukomesha vita na Urusi. 

Usitishaji mapigano wakubaliwa, maelfu wahamishwa

Ukraine-Krieg |  Evakuierung aus Mariupol | dreißig Busse unterwegs
Msafara wa mabasi ya kuwahamisha raia kutoka mji wa Mariupol siku ya Jumanne (8 Machi).Picha: President's Office/REUTERS

Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine, Iryna Vereshchuk, alisema wamekubaliana usitishaji wa mapigano kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi 3:00  usiku kupisha uhamishaji wa watu kwenye mji huo, ambao walipelekwa katka mji wa kusini magharibi mwa Ukraine wa Potlava.

Kwa mujibu wa naibu waziri mkuu huyo, kati ya raia 5,000 waliofanikiwa kuwahamisha, 1,700 ni wanafunzi wa kigeni. 

Jeshi la Urusi lilisema watu 723 ndio waliookolewa kutoka mji huo, likiwatambuwa kuwa wengi wao ni wanafunzi wa kigeni kutoka India, China, Jordan na Tunisia.

Lakini operesheni hiyo ya kuwahamisha raia ilitokea baada ya watu 21 kuuawa kwa makombora yaliyovurumishwa usiku wake kwenye mji huo, kwa mujibu wa maafisa wa Ukraine, ambao pia wameripoti mapambano makali kuendelea kwenye maeneo mengine kadhaa ya nchi.

Watu 17 wauawa Ukraine

Ukraine Krieg Russland Kiew Evakuierung
Wanajeshi wa Ukraine wakimbeba mwanamke kwenye kiti cha maringi baada ya kombora kuangukia karibu yake siku ya Jumatatu (Machi 7) katika viunga vya mji mkuu, Kyiv.Picha: Emilio Morenatti/AP Photo/picture alliance

Kwengineko, mamlaka nchini Ukraine zilisema siku ya Jumatano kwamba ndege za kijeshi za Urusi zimefanya mashambulizi mapya kwenye makaazi ya raia katika sehemu za kati na mashariki mwa nchi hiyo usiku wa Jumanne (Machi 8).

Maafisa walisema kuwa watu wawili, mmoja wao mtoto wa miaka saba, waliuawa kwenye mji wa Chuhuiv mashariki mwa Kharkiv, mji wa pili kwa ukubwa nchini humo.

Katika mji wa Malyn ulio kwenye jimbo la Zhytomyr, magharibi mwa mji mkuu Kyiv, watu watano, wakiwemo watoto wawili, waliuawa kwa mashambulizi ya anga ya Urusi.

Makombora mengine yaliripotiwa kutuwa kwenye viunga vya Kyiv, huku maji, chakula na umeme ukikatwa, kwa mujibu wa Yaroslav Moskalenko, afisa anayeratibu huduma za kiutu kwenye jimbo la Kyiv.

Afisa huyo alisema mashambulizi hayo yamefanya iwe shida kuichukuwa miili ya watu watano waliouawa wakati gari yao ilipoangukiwa na kombora na miili mingine 12 kwenye hospitali ya wagonjwa wa akili, ambako pia wagonjwa 200 wamenasa wakiwa hawana chakula wala dawa. 

Umoja wa Mataifa umethibitisha watu 474 wameshauawa nchini Ukraine na wengine 861 kujeruhiwa tangu uvamizi wa Urusi uanze tarehe 24 Februari.

Watu milioni mbili wakimbia Ukraine

Ukraine Krieg mit Russland Sumy
Mwanajeshi wa Ukraine katika mji wa Sumy.Picha: Irina Rybakova/Press Service Of The Ukrainian Ground Forces/REUTERS

Wakati hayo yakijiri, watu milioni mbili, nusu yao wakiwa watoto, wanaripotiwa kuikimbia Ukraine ndani ya kipindi kisichotimia wiki mbili tangu Urusi kuivamia nchi hiyo.

Hayo ni kwa mujibu wa maafisa wa mipakani wa mataifa yanayowapokea wakimbizi hao, katika wakati huu ambapo Ulaya inashuhudia kile kichotajwa kama mzozo mbaya kabisa wa wakimbizi baada ya Vita vya Pili vya Dunia ukikuwa siku hadi siku. 

Kwa upande mwengine, hali ya kibinaadamu ndani ya miji iliyozingirwa na majeshi ya Urusi nchini Ukraine inazidi kuwa mbaya, ukiwemo mji wa bandari wa Mariupol, ambako taarifa zinasema maiti zimezagaa mitaani na matumaini ya kuwahamisha raia yakipotea kwa mara nyengine. 

Maelfu ya watu, hata hivyo, waliweza kuuhama mji wa kaskazini mashariki wa Sumy wakitumia mabasi siku ya Jumanne, wakipitia njia salama ambazo Ukraine na Urusi walikubaliana kwenye duru ya tatu ya mazungumzo siku ya Jumatatu (Machi 7).