1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yakiri huenda udukuzi ukawa umevuka mipaka

Mjahida1 Novemba 2013

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry akiri udukuzi huenda ukawa umekwenda mbali sana, haya yanajiri wakati bado mvutano unaendelea kati ya taifa hilo na mataifa ya ulaya juu ya madai ya udukuzi

https://p.dw.com/p/1AA5e
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John KerryPicha: Getty Images/Chip Somodevilla

Baada ya siku kumi za mvutano juu ya udukuzi huo taarifa ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry ndio ya kwanza ya kukiri kuwa huenda ikawa maafisa wa Ujasusi wa Marekani wamevuka mipaka katika suala hilo la udukuzi.

Kerry pia ametetea mpango huo na kusema kwamba tangu kutokea kwa mashambulizi ya septemba 11 mwaka wa 2001 nchini Marekani, na mashambulizi mengine jijini London na Madrid, Marekani na nchi nyengine ni lazima zisimame pamoja katika kuwadhibiti magaidi ambao nia yao ni kuuwa watu na kushambulia idara za serikali.

Kerry amesema tangu mwaka huo kumekuwa na uchunguzi wa mawasiliano na kukiri kwamba uchunguzi mwengine huenda ulikuwa unavuka mipaka.

Hata hivyo Kerry hakutoa maelezo yoyote juu ya tamko lake hilo, lakini akasema kwamba tukio ambalo kwa sasa linaleta mvutano na washirika wake wa karibu kama Ujerumani halitarejelewa tena.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, na Rais wa Marekani Barrack Obama
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, na Rais wa Marekani Barrack ObamaPicha: Getty Images

Waziri huyo wa nchi za nje wa Marekani licha ya kukiri kwamba huenda udukuzi unaofanywa ukawa unapita mipaka pia amehakikisha kuwa hakuna mtu yoyote anayehujumiwa katika mpango huo wa kukusanya habari.

Wiki hii Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alihamaki na kumuweka sawa Rais wa Marekani Barrack Obama kuhusu madai kwamba maafisa wa Ujasusi wa Marekani wamekuwa wakichunguza mawasiliano yake ya simu na kusema kwamba iwapo hilo litathibitishwa basi hii itaondoa imani ya Ujerumani kwa Marekani.

Wabunge wa Ulaya wataka kujua zaidi juu ya udukuzi

Siku ya Jumatano wiki hii kundi la wabunge wa Ulaya walikuwa mjini Washington Marekani kutaka kujua zaidi juu ya uchunguzi wa Marekani kwa washirika wake.

Huku hayo yakiarifiwa kamati ya baraza la seneti inayohusika na masuala ya Ujasusi nchini Marekani ilipitisha mswada hapo jana unaodhibiti kiwango cha kufanya uchunguzi kwa kutumia vyombo vya elektroniki lakini ikakubali udukuzi huo kuendelezwa.

Katika mswada huo imekubalika uchunguzi wa mawasiliano unaweza kufanyika kwa miaka mitano tu. Mswada huo umepingwa vikali na kampuni za teknologia pamoja na makundi ya kiraia nchini Marekani.

Mfanyakazi wa zamani wa shirika la NSA Edward Snowden
Mfanyakazi wa zamani wa shirika la NSA Edward SnowdenPicha: picture alliance/AP Photo

Wakati huo huo mbunge mmoja wa Ujerumani amekutana na mfichua siri za kijasusi za Marekani Edward Snowden mjini Moscow, na kusema mfanyakazi huyo wa zamani wa shirika la Ujasusi la NSA yuko tayari kuja Ujerumani kusaidia katika uchunguzi wa udukuzi wa mawasiliano ya simu ya mkononi ya Kansela Angela Merkel.

Hans-Christian Stroebele mbunge wa upinzani wa chama cha walinzi wa mazingira ameliambia shirika la habari la Ujerumani la ARD kwamba inaonekana Edward Snowden anajua mengi juu ya sakata hiyo na kusema kuwa atatoa habari zaidi leo katika barua aliyoiandikia serikali ya Ujerumani na mwendesha mashtaka mkuu wa Ujerumani.

Bunge la Ujerumani hata hivyo limepanga kufanya kikao maalum Novemba 18 kuzungumzia juu ya udukuzi huo huku chama cha walinzi wa mazingira kikitaka mashahidi kama Edward Snowden kuitwa kueleza wanachokijua juu ya udukuzi huo.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu