1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Marekani yaliona puto la pili la ujasusi la China

4 Februari 2023

Wizara ya Ulinzi ya Marekani imesema imeliona puto la ujasusi la China katika anga ya Amerika Kusini, ikiwa ni siku moja baada ya puto kama hilo kuonekana kwenye anga ya Marekani.

https://p.dw.com/p/4N68F
Chinas Spionageballon über den USA
Picha: Larry Mayer/Billings Gazette/AP/picture alliance

Tukio hilo lilisababisha kufutwa kwa ziara ya Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Antony Blinken mjini Beijing. Pentagon imesema puto la kwanza sasa linaelekea mashariki katika anga ya katikati mwa Marekani, ikiongeza kuwa haliwezi kudunguliwa kwa sababu za kiusalama.

Muda mfupi kabla ya uamuzi wa Blinken kuifuta ziara yake, iliyolenga kutuliza mvutano kati ya nchi hizo mbili, China ilitoa taarifa ya nadra ya kuonyesha kujutia tukio la puto la kwanza. Ilidai kuwa upepo ulisukuma katika anga ya Marekani kile lilichokiita chombo cha angani cha kiraia. Lakini serikali ya Rais Joe Biden imekielezea kuwa ni puto kubwa la kutumika katika ujasusi. Wizara ya Mambo ya Kigeni ya China imesema leo kuwa ziara ya Blinken haitofanyika kama ilivyopangwa.