Marekani yaonya kuhusu vikwazo kwa mradi wa Nord Stream 2
24 Machi 2021Blinken amesema pia kwamba Marekani inapinga waziwazi ujenzi wa njia hiyo ya usafirishaji gesi.
Akizungumzia kwa mara nyengine hofu ya Rais Joe Biden kuhusiana na njia hiyo ya usafirishaji gesi kutoka Urusi hadi Ujerumani, Blinken amemwambia Waziri Heiko Maas katika mkutano wa faragha kuwa, kampuni zinazohusika katika mradi huo huenda zikawekewa vikwazo hasa kuelekea mwishoni mwa ujenzi wa mradi huo.
Kampuni zinazojenga huenda zikawekewa vikwazo
Maafisa na wanadiplomasia wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa Ujerumani imekuwa ikiuomba utawala mpya wa Marekani ulio chini ya Joe Biden kuchukua uamuzi mzuri katika mradi huo wa kusafirisha gesi ya Urusi kuelekea Ulaya kwa kuwa unaelekea kukamilika.
"Nimeweka wazi kwamba kampuni zinazohusika katika ujenzi ziko kwenye hatari ya kuwekewa vikwazo na Marekani. Njia hioyo ya kusafirisha gesi inaigawanya Ulaya, inaiweka Ukraine na Ulaya ya kati katika hali ya kutapeliwa na Urusi, inakwenda kinyume kabisa na malengo ya Ulaya kuhusiana na kawi," alisema Blinken.
Urusi inasema Nord Stream 2 ambao ni mradi wa dola bilioni 11 unaoongozwa na kampuni kubwa ya nishati ya Urusi Gazprom, ni mradi wa kibiashara ila tawala kadhaa za Marekani zimeupinga mradi huo na Ulaya imeahidi kupunguza kuitegemea sana nishati ya Urusi.
Ilikuwa muhimu kuweka wazi kwa Ujerumani kuwa Marekani inapinga
Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya zilizoko mashariki mwa bara hilo kama Poland zinasema mradi wa Nord Stream 2 ni sehemu ya hatua za kiuchumi na kisiasa za Urusi kwa ajili ya kuzitapeli nchi za Ulaya na kuendea kinyume mahusoani ya transatlantic.
"Nilichomwambia Maas ni kwamba, tutaendelea kutazama mambo yanavyokwenda ili kukamilisha au kuidhinisha ubora wa mradi huo na iwapo hilo litafanyika basi tutaamua jinsi ya kuweka vikwazo," alisema Blinken.
Blinken alisema ilikuwa muhimu kuupeleka ujumbe moja kwa moja kwa Maas ili "kuweka wazi msimamo wa Marekani na kuhakikisha kwamba hakuna mkanganyiko wa aina yoyote."
Shirika la habari la Reuters liliripoti mnamo Februari 24 kwamba kampuni 18 ziliacha kufanya kazi katika mradi huo kwa hofu ya kuwekewa vikwazo.