Marekani yapiga hatua katika uchomaji chanjo ya corona
19 Aprili 2021Tukianzia Marekani, nchi ambayo imeathirika vibaya zaidi na maambukizi pamoja na vifo kutokana na Covid-19 duniani, Kituo cha Kudhibiti Magonjwa nchini humo CDC kinasema kwa sasa nusu ya watu wazima nchini humo wameshachomwa dozi moja ya chanjo ya Covid-19, hiyo ikiwa ni watu milioni 130 walio na umri wa miaka 18 na zaidi.
Lakini licha ya kuongoza juhudi za utoaji chanjo, idadi ya maambukizi imekuwa ikiongezeka katika siku za hivi majuzi jambo lililompelekea mshauri mkuu wa janga hilo Dokta Anthony Fauci kusema kwamba Marekani bado iko katika hali mbaya.
Hali ikoje katika Mji Mkuu wa India?
Juhudi za utoaji wa chanjo ya Johnson & Johnson zimekumbwa na kizingiti kwa mara nyengine baada ya visa nadra vya kuganda kwa damu kuripotiwa kwa wanawake wengine sita. Kwa sasa utoaji wa chanjo hiyo umesitishwa na wataalam wanachunguza visa hivyo na uamuzi kuhusiana na kuendelea kutumika kwake unatarajiwa baadae wiki hii.
"Makadirio yangu ni kwamba tutaendelea kuitumia kwa kiasi fulani. Sidhani kama watafutilia mbali matumizi yake kabisa, sifikiri kama hilo litafanyika," alisema Fauci.
Kwengineko shughuli katika Mji Mkuu wa India New Delhi zitafungwa kuanzia usiku wa Jumatatu baada ya nchi hiyo kuandikisha zaidi ya maambukizi 270,000 hapo Jumapili na zaidi ya vifo 1,600, hiyo ikiwa ni rekodi mpya ya maambukizi na vifo kwa siku moja. Miji iliyoathirika zaidi imeweka sheria kali za kudhibiti maambukizi.
Nako barani Ulaya kamishna wa masoko ya ndani wa Umojawa Ulaya Thierry Breton amedokeza kuwa huenda umoja huo usiagize tena chanjo za Astrazeneca baada ya chelewa chelewa ya kuwasilisha dozi za kwanza. Umoja wa Ulaya awali ulikuwa umeagiza dozi milioni 120 kwa ajili ya nchi zake 27 wanachama ila kampuni hiyo iliwasilisha dozi milioni 30 tu.
Waisraeli sasa wakubaliwa kutembea bila barakoa
Huku hayo yakiarifiwa baadhi ya nchi za Ulaya zimeanza kulegeza vikwazo huku Ureno ikiondoa marufuku ya ndege kutoka Brazil nayo Uswisi kuanzia Jumatatu inakubali kufunguliwa kwa migahawa na hata vyuo vikuu.
Kwengineko Australia na New Zealand wamepata kionjo tu cha jinsi maisha ya kawaida yalivyo tena, baada ya mipaka ya nchi hizo kufunguliwa na raia wake kuruhusiwa kusafiri baina ya nchi hizo mbili bila kuingia karantini wanapowasili.
Waisraeli nao kwa mara ya kwanza Jumapili baada ya mwaka mmoja walitembea mitaani bila barakoa kufuatia zaidi ya asilimia 50 ya watu nchini humo kuchomwa chanjo. Miezi michache tu iliyopita, Israel ilikuwa na mojawapo ya kiwango kikubwa zaidi cha maambukizi duniani ila hali ilibadilika pakubwa baada ya kuingia kwenye mkataba na kampuni ya Pfizer na BioNTech iliyowasilisha chanjo nchini humo kwa wingi.