1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSomalia

Marekani yapongeza mkataba mpya kati ya Ethiopia na Somalia

13 Desemba 2024

Marekani imepongeza makubaliano yaliyofikiwa na Somalia na Ethiopia ya kumaliza mivutano ya kikanda, iliyochochewa na shinikizo la Ethiopia la ufikiaji salama wa baharini.

https://p.dw.com/p/4o5ae
Antony Blinken, waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani
Blinken amezihimiza Somalia na Ethiopia kuimarisha ushirikiano wao juu ya maslahi ya usalama wa pande zote.Picha: Andrew Caballero-Reynolds/Pool Photo via AP/picture alliance

Katika taarifa, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, amesema Marekani inapongeza Azimio la Desemba 11 kati ya Somalia na Ethiopia linalothibitisha tena uhuru wa kila nchi, umoja, na uadilifu wa kimaeneo.

Blinken ameongeza kuwa Marekani ilikuwa inatazamia mazungumzo ambayo yangeelezea ufikiaji wa bahari wa Ethiopia huku ikiheshimu uadilifu wa eneo la Somalia.

Blinken amezihimiza nchi hizo mbili kuimarisha ushirikiano wao juu ya maslahi ya usalama wa pande zote, hasa mapambano dhidi ya kundi la al-Shabaab.

Waziri huyo pia ameishukuru Uturuki kwa kusimamia makubaliano hayo mapya.

Taarifa hiyo imetolewa wakati Blinken alipokuwa katika mazungumzo na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan mjini Ankara kuhusu hali nchini Syria.

AU wazitaka Somalia na Ethiopia kutekeleza makubaliano yao

Umoja wa Afrika nao umezihimiza Ethiopia na Somalia kutekeleza "bila kuchelewa" makubaliano hayo  'muhimu yaliyofikiwa Desemba 11' yenye lengo la kumaliza mvutano kati ya mataifa hayo majirani.

Nchi hizo mbili zimekuwa na mzozo tangu Ethiopia isiyo na bandari ilipofikia makubaliano mwezi Januari na eneo lililojitenga na Somalia la Somaliland, kukodisha eneo la pwani kwa ajili ya ujenzi wa bandari na kambi ya kijeshi. Kitendo kilichoichukiza Somalia na hivyo kuzusha hofu ya kuzuka kwa mzozo wa kikanda.