Marekani yasema IS imezuiwa
24 Oktoba 2014Inaripotiwa kuwa hadi sasa Marekani na washirika wake wameshafanya mashambulizi 6,600 ya kila aina dhidi ya wanamgambo wa IS, wakiangusha zaidi ya mabomu 1,700, yaliyouwa watu 553, ambapo 521 ni wapiganaji wa kigeni, na waliobakia raia wa kawaida.
Lakini mafanikio ya operesheni hiyo ya anga isiyofahamika ukomo wake yanahojika. Kwa upande wake, Ikulu ya Marekani inasema IS imeharibiwa vibaya kwa mashambulizi hayo, lakini wakosoaji wanasema mafanikio ya kundi hilo kwenye uwanja wa mapambano ni makubwa licha ya kushambuliwa vikali na madola makubwa duniani.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Chuck Hagel, amekiri kwamba kuna matokeo mchanganyiko kwenye vita hivi, lakini akasema: "Ninaamini kuwa mkakati wetu dhidi ya IS unafanya kazi."
Kwenyewe Kobane, jana wanamgambo wa IS walifanya mashambulizi mapya na kuchukuwa vijiji kadhaa magharibi mwa mji huo, kwa mujibu wa Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu la Syria.
Wapiganaji wa Kikurdi ndio tegemeo
Matumaini makubwa ya kulishinda kundi hilo yamewekwa kwa wapiganaji wa Kikurdi kwenye mji wa Kobane, Syria na wale wanaotoka jimbo la Kurdistan, Iraq, ambao kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa wamepambana kwa ushujaa mkubwa.
Afisa mmoja wa wizara ya ulinzi ya Marekani kwenye kituo kinachoongoza mashambulizi ya anga dhidi ya IS, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wapiganaji hao wa Kikurdi wanaonekana watafanikiwa. Lakini hilo litakuwa tu, endapo watapata msaada waliohadiwa na wenzao kutoka Iraq.
Juzi Jumatano, wabunge wa jimbo la Kurdistan kaskazini mwa Iraq, walipiga kura kuidhinisha kutumwa kwa vikosi vya peshmerga baada ya Uturuki kusema ingelikubali kuwaruhusu wapiganaji 200 kuingia Kobane kupitia mpaka wake, ambako IS wanakisiwa kuwa na wapiganaji 1,000.
Jeshi la Iraq haliko tayari sasa
Maafisa wa Marekani hivi leo wametoa taarifa ikisema kwamba jeshi la Iraq litachukuwa miezi kadhaa kabla ya kuwa na uwezo wa kufanya mashambulizi ya kuitwaa miji iliyotekwa na IS. Kwa mujibu wa maafisa hao, kwa sasa kinachoweza kufanywa na jeshi hilo ni mashambulizi madogo madogo tu, na kwamba linahitaji muda zaidi wa kujipanga kwa operesheni kubwa.
Katika siku za karibuni hata mji mkuu Baghdad umekuwa ukishuhudia mashambulizi ya mabomu yanayofanywa na IS. Kundi hilo lililotangaza kuanzisha utawala wa Kiislamu kwenye maeneo lililoyateka nchini Iraq na Syria mnamo mwezi Juni, linaelezewa kuwa tajiri kabisa miongoni mwa makundi mengine ya kigaidi duniani, likiwa linaingiza dola milioni moja kwa siku kutokana na biashara ya mafuta.
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf