Marekani yasema jeshi la Myanmar limefanya mauaji ya halaiki
21 Machi 2022Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wamesema, Marekani kutambua hilo kunafungua fursa kwa Majenerali wa jeshi la Myanmar waliomwaga damu za watu wa jamii ya Rohingya kuwajibishwa.
Uamuzi huo wa Marekani, wanasheria wanasema utaongeza shinikizo kwa jeshi la Myanmar ambalo sasa ndilo linaloshikilia madaraka, kuwajibishwa kwa makosa hayo.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken atatangaza uamuzi huo leo Jumatatu kwenye jumba la makumbusho la Holocaust mjini Washington, ambapo maafisa wa Marekani wanasema lina maonyesho ya maangamizi, madhila na mateso waliyoyapitia watu wa jamii ya Rohingya.
Soma pia: Save the Children yasema wafanyakazi wake wameuawa Myanmar
Tangazo hilo linatokea karibu miezi 14 baada ya Blinken kuchukua wadhifa wa Waziri wa mambo ya nje na kuahidi kufanya uchunguzi upya juu ya vurugu nchini Myanmar.
Jeshi la Myanmar laanzisha oparesheni ya kijeshi dhidi ya "magaidi"
Jeshi la Myanmar lilianzisha oparesheni ya kijeshi mnamo mwaka 2017 ambayo ilisababisha watu wapatao 730,000 wengi wao kutoka jamii ya waislamu wachache wa Rohingya kutoroka makwao na kukimbilia katika nchi jirani ya Bangladesh ambako walisimulia madhila waliyoyapitia ikiwemo mauaji, ubakaji na baadhi yao kuchomwa moto.
Mnamo mwaka 2021, jeshi la Myanmar lilichukua madaraka kwa njia ya mapinduzi. Maafisa wa Marekani walikusanya ushahidi katika juhudi za kutambua haraka uzito wa makosa yaliyofanywa na jeshi la Myanmar, lakini Waziri wa mambo ya nje wa Marekani wakati huo Mike Pompeo alikataa kufanya uamuzi. Hata hivyo tofauti na mwenzake, Blinken aliamuru uchunguzi wa uhakika na wa kisheria, maafisa wa Marekani wameliambia shirika la habari la Reuters japo kwa sharti la kutotajwa majina.
Uchunguzi huo umehitimisha kuwa jeshi la Myanmar lina kesi ya kujibu, kwani linafanya mauaji ya halaiki na Marekani inaamini kwamba uamuzi rasmi wa kuafiki makosa hayo utaongeza shinikizo la kimataifa kuliwajibisha jeshi la Myanmar.
Soma pia:Umoja wa Mataifa wahofia uhalifu mkubwa kutendeka Myanmar
Maafisa katika ubalozi wa Myanmar mjini Washington pamoja na msemaji wa jeshi hawakujibu barua ya kuwataka kuzungumzia juu ya suala hilo. Jeshi la Myanmar limekanusha kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Rohingya, ambao wananyimwa uraia wa Myanmar na badala yake jeshi hilo linajificha chini ya kivuli cha kuendesha oparesheni dhidi ya magaidi.
Ujumbe wa uchunguzi wa Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 2018, ulisema kuwa katika oparesheni hiyo ya jeshi la Myanmar, kulijumuishwa vitendo vya mauaji ya kimbari japo Marekani wakati huo ilisema vitendo vya jeshi hilo vilikuwa ni utakaso wa kikabila, neno ambao halina ufananuzi kamili chini ya sheria ya uhalifu wa kimataifa.
Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wanaamini kuwa, kwa Marekani kutambua kuwa mauji ya kimbari yalifanywa na jeshi la Myanmar kunaweza kuweka hai juhudi za kuwawajibisha majenerali wa jeshi la Myanmar.
Hata hivyo Myanmar imekanusha kuhusika na mauaji ya halaiki.