1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yasisitiza itaiadhibu Syria

31 Agosti 2013

Marekani imedhihirisha wazi kuwa itaiadhibu Syria kwa shambulio la Damascus ambapo zaidi ya watu 1,400 waliuawa huku wachunguzi wa umoja wa Mataifa wakikamilisha uchunguzi wao na kuondoka Syria leo (31.08.2013).

https://p.dw.com/p/19ZMe
Picha: picture alliance/AP Photo

Rais wa Marekani Barrack Obama amesema hawawezi kukubali ulimwengu ambao unaruhusu wanawake, watoto na raia wasio na hatia kuuawa katika kiwango kikubwa.

Obama amesema Marekani bado inapanga hatua za kijeshi lakini hajaeleza ni lini hasa hatua hizo zitachukuliwa.Matamshi yake yanakuja huku nchi yake ikitoa ripoti ya kijasusi inayoonyesha utawala wa Syria ulishambulia eneo karibu na mji mkuu Damasacus na kuwaua watu 1,429 wakiwemo watoto 426.

Obama amesema ulimwengu una wajibu wa kuhakikisha kuwa hakuna matumizi ya silaha za kemikali na kulishutumu baraza la usalama la umoja wa mataifa kwa kushindwa kuafikiana kuhusu hatua gani ichukuliwe dhidi ya Syria.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry hapo jana alizungumza na mawaziri wenzake kutoka Uingereza, Misri, Ujerumani, Uholanzi, New Zealnd, Saudi Arabia na Milki za falme ya kiarabu pamoja na katibu mkuu wa umoja wa nchi za kiarabu.

Ufaransa imeunga mkono msimamo wa Marekani kwa kusema ujumbe mzito unapaswa kufikishwa kwa utawala wa Rais Bashar al Assad. Bunge la Uingereza lilipinga nchi hiyo kujihusisha na hatua za kijeshi dhidi ya Syria baada ya kupiga kura kupinga azma ya waziri mkuu David Cameron.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akizungumzia hali nchini Syria kufuatia shambulio la gesi ya sumu
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akizungumzia hali nchini Syria kufuatia shambulio la gesi ya sumuPicha: Reuters

Urusi ambayo ni mshirika mkubwa wa Syria imetilia shaka uchunguzi wa kijasusi wa Marekani kuhusu shambulio hilo la tarehe 21 mwezi huu la gesi ya sumu na kuonya kutochukuliwa hatua zozote za kijeshi kabla ya kuidhinishwa na umoja wa Mataifa.

Wachunguzi wakamilisha uchunguzi Damascus

Umoja wa Mataifa hapo jana ulitangaza kuwa wachunguzi wao wamekamilisha kukusanya uchunguzi wao mjini Damascus na huenda ikachuka wiki kadhaa kwa wao kutathmini na kuwasilisha ripoti kamili kuhusu uchunguzi huo.

Kundi hilo la wachunguzi limeonekana leo likiondoka katika hoteli waliyokuwa wakikaa mjini Damascus katika msafara wa magari ulionekana katika barabara kuu inayoelekea nchi jirani ya Lebanon.

Wachunguzi hao wameahidi kuharakisha kutoa ripoti yao na wanatarajiwa kuripoti kwa katibu mku wa umoja huo Ban ki Moon ambaye amezihimza nchi za magharibi kuruhusu uchunguzi huo kutathiminiwa kwa kuwa na subira.

Kerry amesema kushindwa kuchukua hatua dhidi ya Syria kutakengeuka desturi ya kupiga marufuku matumzi ya silaha za kemikali na kuzipa nguvu Iran na kundi la wanamgambo la Hezbollah kuzitumia.

Je Marekani itaungwa mkono na nchi nyingine?

Marekani imelazimika kuangalia kwingine kupata uungwaji mkono baada ya bunge la Uingereza kupinga kujihusisha kwa nchi hiyo kijeshi na Syria. Ujerumani na Canada zimesema bayana kuwa nazo hazitashiriki katika hatua za kijeshi lakini Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema hatua ya Uingereza haitabadili msimamo wa serikali yake kuhusu umuhimu wa kuvamiwa kwa Syria.Uturuki nchi jirani na Syria pia inaiunga mkono Marekani.

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wakiondoka hotelini mwao mjini Damascus
Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wakiondoka hotelini mwao mjini DamascusPicha: picture-alliance/dpa

Urusi na Iran zimeionya Mareknai na nchi za magharibi kutochukua hatua zozote za kijeshi badala yake kutafutwe suluhu la kisiasa kutatua mzozo wa Syria.

Marekani inajikuta katika hali tete hasa baada ya vita vya Iraq na Afghanistan ambavyo kuhusika kwake kunaonekana kutokuwa na tija badala yake kuziacha nchi hizo katika hali mbaya zaidi.

Kulingana na umoja wa Mataifa,kiasi ya watu 100,000 wameuwa katika vita hivyo vya wenyewe Syria tangu vianze zaidi ya miaka miwili iliyopita na mamilioni wengine wamekuwa wakimbizi.

Mwandishi:Caro Robi/Afp/Reuters

Mhariri: Josephat Charo