Marekani yatuma wanajeshi, mzozo wa Ukraine ukizorota
3 Februari 2022Marekani inataraji kupeleka wanajeshi takriban 3,000 nchini Poland na Romania kama moja ya mkakati wa kulilinda eneo la mashariki mwa Ulaya dhidi ya kitisho cha kusambaa kwa mzozo kufuatia hatua ya Urusi ya kurundika wanajeshi wake karibu na mpaka wa Ukraine.
Soma Zaidi: Nyaraka zavuja, zaonyesha Marekani kutaka kukubaliana na Urusi
Rais Joe Biden wa Marekani amesema kupelekwa kwa wanajeshi hao kunakwenda sambamba na kile alichowahi kumwambia rais Vladimir Putin wa Urusi kwamba, iwapo ataendelea kuchukua hatua za uchokozi, Marekani itahakikisha inawasaidia washirika wake wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO pamoja na Ulaya Mashariki, hii ikiwa ni kulingana na taarifa za baadhi ya vyombo vya habari kwenye kurasa zao za twitter.
Msemaji wa wizara ya ulinzi ya John Kirby amesema Marekani ilitakiwa kutuma ishara kali kwa Putin na kuwa wakweli mbele ya ulimwengu kwamba NATO ina umuhimu mkubwa kwa taifa hilo na hata kwa washirika wake.
Waziri wa ulinzi wa Poland Mariuzs Blaszczak amesema kupelekwa kwa wanajeshi hao wa Marekani ni ishara thabiti na ya mshikamano. Katibu mkuu wa jumuiya hiyo Jens Stoltenberg pia ameukaribisha uamuzi huyo akisema muungano huo unaushughulikia mzozo huo kwa kujilinda na sambamba na hatua zinazochukuliwa na Urusi.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema jana kwamba, atafanya jitihada za kuzungumza na Biden kuhusiana na mzozo huo wa ukraine, lakini hakutaka kuthibitisha iwapo atakutana na rais Putin ili kujaribu kuangazia hatua za kuondoa wanajeshi wake kwenye mpaka wa Ukraine.
Macron alitoa matamshi hayo baada ya kuwasili katika mji wa Tourcoing, kaskazini mwa Ufaransa kuhudhuria mkutano usio rasmi wa mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya na kuongeza kuwa ana wasiwasi mkubwa kuhusu hali ilivyo nchini Ukraine.
"Nina wasiwasi sana na hali ya Ukraine. Nimeongeza majadiliano kati yangu na wenzangu wa Ulaya, na mara nyingi na rais Putin na rais Zelensky na nitazungumza katika kipindi cha saa chache zijazo na rais Biden, kwa vyovyote vile tutajaribu kutafuta msingi wa pamoja."
Juhudi za kusaka suluhu kwa njia ya kidiplomasia zinaendelea, licha ya baadhi ya mataifa ya magharibi kuendelea kuyaona masharti ya kiusalama ya Urusi kama yasiyo ya msingi, na Moscow yenyewe ikiwa haina nia ya kuyaondoa masharti hayo.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan naye anapanga kukutana na rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine baadae leo baada ya taifa hilo kujiingiza kama mpatanishi katika juhudi za kupunguza mzozo, huku kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akisema atakutana na rais Putin mjini Moscow hivi karibuni, ingawa hakukutajwa siku hasa watakayokutana.
Mwandishi: RTRE