Marekani yawashinikiza washirika wa NATO kuhusu ulinzi
28 Aprili 2018Aliyasema hayo katika mkutano wa mawaziri wa kigeni wa NATO siku moja tu baada ya kuidhinishwa kuwa mwanadiplomasia mpya mkuu wa Donald Trump
Pompeo, ambaye amehudumu kama mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani – CIA katika serikali ya Trump, alifunga safari yake ya kwanza ya kigeni akiwa waziri saa chache tu baada ya kuidhinishwa katika wadhifa huo.
Punde baada ya kuwasili Brussels, hakupoteza muda kabla ya kurudia wito wa Marekani kwa mataifa wanachama wa NATO kugawana jukumu la ulinzi.
Akizungumza na wanahabari, Pompeo alisema mataifa ya Ulaya lazima yabebe majukumu yanayohitajika kwa ajili ya ulinzi wao na kuwafafanulia wananchi wao ni kwa nini ni muhimu kutimiza majukumu yao ya matumizi ya ulinzi
Rais wa Marekani Donald Trump kila mara huwashambulia washirika wa NATO kwa kutotimiza ahadi zao za bajeti ya ulinzi ya NATO. Marekani kwa ndio mchangiaji mkubwa wa bajeti ya ulinzi ya NATO.
Katika mwaka wa 2014, Nchi kadhaa za NATO, ikiwemo Ujerumani, zilikubali kutumia asilimia mbili ya bajeti ya ulinzi kutoka patojumla la nchi ifikapo mwaka wa 2024
Pompeo amesema kuwa Ujerumani haitimizi malengo yake ya bajeti. Ijapokuwa Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Heiko Maas alisisitiza kuhusu juhudi za kiutu zinazofanywa na nchi yake nchini Syria na Iraq, akiongeza kuwa serikali mpya kwa sasa inaandaa bajeti, hakuahidi kuwa itapelekea kuongeza matumizi ya ulinzi.
Katika mwaka wa 2017, Ugiriki, Uingereza na Estonia zilijiunga na Marekani katika kutimiza lengo la asilimia mbili ya matumizi ya ulinzi.
Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg alimkaribisha Pompeo, akisema ziara yake ya mapema baada ya kuteuliwa inadhihirisha umuhimu wa jumuiya hiyo na umuhimu ambao Marekani inauweka kwa jumuiya hiyo.
Mawaziri wa kigeni pia waliijadili Urusi wakati wa mkutano huo, wakithibitisha mkakati wa NATO wa kutaka kuizuia Urusi dhidi ya tabia yake ya kuyumbisha. Kuhusu Afghanistan, Stoltenberg amesema mawaziri hao waliikaribisha hatua isiyokuwa ya kawaida ya Rais Ashraf Ghani ya kufanya mazungumzo ya Amani na Taliban. Aidha walilaani vikali matumizi ya silaha za sumu yanayofanywa na serikali ya Syria na kuelezea kuunga mkono mazungumzo ya Amani yanayoongozwa na Umoja wa Mataifa.
Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Sekione Kitojo