1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Yumkini Shireen aliuwawa kwa risasi ya Israel

4 Julai 2022

Maafisa wa Marekani wamefikia hitimisho leo Jumatatu kuwa risasi iliyomuua mwandishi habari wa Al-Jazeera Shireen Abu Akleh huenda ilifyetuliwa na vikosi vya Israel.

https://p.dw.com/p/4DdzT
Frankreich I Nach Tod von Journalistin im Westjordanland - Proteste
Picha: Ilia Yefimovich/dpa/picture alliance Ilia Yefimovich/dpa

Taarifa hizo zimetolewa na Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani ingawa imesema "hakuna sababu ya kuamini" kwamba kushambuliwa kwake kulikuwa kwa makusudi.

Ugunduzi huo uliotolewa na msemaji wa wizara hiyo Ned Price unakuja baada ya Marekani kusema hapo kabla kwamba uchunguzi  uliofanywa na wataalamu huru wa milipuko haukuweza kufikia hitimisho la uhakika juu ya upande hasa uliofyetua risasi hiyo.

"Wataalamu wa milipuko wamebaini risasi ilikuwa imeharibika vibaya, na hilo limezuia kutoka na himitisho la uhakika" ya nani hasa aliyefyetua risasi, amesema Price katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Mkasa uliozusha mvutano mkubwa Mashariki ya Kati 

Trauer um Shireen Abu Akleh
Picha: Muammar Awad/Xinhua/IMAGO

Abu Akleh, mwandishi mkongwe na mashuhuri katika ulimwengu wa kiarabu alipigwa risasi na kuuwawa mnamo Mei 11 wakati akiripoti operesheni ya kijeshi ya vikosi vya Israel katika mji wa Jenin uliopo Ukingo wa Magharibi.

Mashuhuda wa Kipalestina ikiwemo wafanyakazi wenzake wanasema vikosi vya Israel ndiyo vilimuua na hakukuwa na makundi ya wapiganaji wenye silaha kwenye eneo la mkasa.

Israel kwa upande wake inasema aliuwawa wakati wa makabiliano magumu na wanamgambo wa Kipalestina na ni uchunguzi pekee wa kimaabara wa risasi iliyotolewa mwilini kwa mwandishi huyo habari ndiyo unaweza kuthibitisha iwapo ilifyetuliwa na jeshi la Israel au wanamgambo wa Kipalestina.

Nchi hiyo imekanusha kwamba mwandishi huyo alilengwa kwa makusudi lakini imesema huenda askari wa Israel alipiga risasi kwa bahati mbaya wakati wa kurushiana risasi na mwanamgambo mwenye silaha.

Palestina yasisitiza Shireen alilengwa na vikosi vya Israel 

Maafisa wa usalama wa Marekani wametathmini matokeo ya uchunguzi uliofanywa na pande zote mbili yaani Israel na Palestina na wamehitimisha kwamba "risasi kutoka jeshi la Israel ndiyo huenda ilisababisha kifo cha Shireen Abu Akleh" amesema Price.

Jerusalem | Beisetzung Shireen Abu Akleh, Journalistin Al-Jazeera
Maelfu walijitokeza kwenye mazishi ya ShireenPicha: Ahmad Gharabli/AFP/Getty Images

Marekani imesema haijabaini sababu yoyote ya kuamini kwamba mkasa huo ulikuwa wa kukusudia lakini badala yake ilikuwa ni matokeo ya mazingira yasiyotarajiwa kwenye uwanja wa mapambano wakati wa operesheni ya jeshi la Israel huko Jenin.

Tangu kutokea kisa hicho Mamlaka za Palestina zimekitaja kifo cha Akleh ambaye alikuwa akiripoti uvamizi wa Israel katika eneo la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu, kama tukio la mauaji la vikosi vya Israel.

Wakati akipigwa risasi hiyo Abu Akleh alikuwa akiripoti kutoka kambi ya Jenin akiwa amevalia kizibao cha kumkinga na risasi na ambacho kilikuwa na maandishi ya wazi kabisa yanayoonesha ni mwandishi wa habari, alikuwa pia na kofia ngumu kichwani.

Kuuwawa kwake kuliamsha ulimwengu wa kiarabu na lawama ya kimataifa. Kulikuwa na maandamano makubwa huko Palestina na hata Uturuki, yalifika pia Sudan na kwengineko ulimwenguni.