Mark webber kuihama Red Bull, Formula One
28 Juni 2013Kampuni ya Red Bull imesema haitamtaja dereva atakayejaza nafasi ya Webber kwa sasa hadi mwishoni mwa msimu. Dereva wa Lotus Kimi Raikkonen, bingwa wa ulimwengu mwaka wa 2007, anapigiwa upatu kuchukua nafasi hiyo.
Webber mwenye umri wa miaka 36, yuko katika mwaka wake wa 12 wa F1 na ndiye dereva mwenye umri mkubwa zaidi katika mashindano hayo kwa sasa. Hajashinda mbio zozote msimu huu wa mwaka 2013 na yuko katika nafasi ya tano ya orodha ya madereva bora.
Kiongozi wa kampuni ya Red Bull Christian Horner amesema Webber alifanya tathmini ya muda mrefu kabla ya kufanya uamuzi huo ambao bila shaka ulikuwa ni mgumu. Webber alijiunga katika Formula One mwaka wa 2002 kama sehemu ya kikosi cha Minardi cha Muaustralia mwenzake Pau Stoddart. Alijiunga na Red Bull mwaka wa 2007 na ameshinda mataji tisa ya Grand Prix na kikosi hicho, lakini kila mara amekuwa akiendesha katika kivuli cha mwenzake mshindi mara tatu wa ulimwengu Sebastian Vettel.
Kumekuwepo na uvumi kuwa msimu huu ungekuwa wa mwisho kwa Webber na kikosi cha Red Bull tangu mkondo wa Malaysian Grand Prix mwezi Machi, wakati Vettel alipopuuza maaguzo ya kikosi chaeo na kumpiku Muastralia huyo na kushinda mbio hizo. Webber hata hivyo amesisitiza kuwa utata huo haukuchangia lolote katika uamuzi wake wa kuondoka katika F1 akisema kuwa alikuwa na mpango wa kibinafsi.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri: Yusuf Saumu