Mashambulio ya kigaidi mjini Mumbai
2 Desemba 2008Baada ya mashambulio ya kigaidi ya hivi karibuni yaliotokea katika mji mkubwa wa kibiashara wa India, Mumbai, na yaliosababisha kuuwawa watu 183, serekali ya nchi hiyo inajikuta katika mbinyo mkubwa, ikilaumiwa kwamba haikuweza kukabiliana vizuri na mzozo huo na kwamba idara zake za ujasusi zilizubaa. Hasira kubwa za wananchi hata zimesababisha kujiuzulu waziri wa mambo ya ndani wa serekali kuu, Shivraj Patil. Wakaazi wa mji huo waliokasirika waliandamana mbele ya Hotel ya Taj Mahal ilioungua kabisa kwa moto kutokana na mapigano makubwa baina ya magaidi na polisi. Wageni wa hoteli hiyo, wakiwemo wenye uraia wa kigeni, pamoja magaidi,walikufa hapo. Polisi ilitajwa inabeba sehemu kubwa ya dhamana ya yale yaliotokea. Raia mmoja alisema hivi:
"Tungependa kuuliza: nini hasa serekali imefanya? kwa nini mfumo wetu haufanyi kazi? Nini kilichokwenda kombo? Baada ya shambulio la bomu katika hoteli ya Marriot huko Pakistan, idara za ujasusi zilizubaa kabisa"
Tangu mwaka 2004 wameuwawa zaidi ya watu alfu nne huko India kutokana na mashambulio ya kigaidi, kila mji mkubwa ukijionea mashambulio: Ni Iraq tu iliotia fora. Lakini ubaya zaidi ni kwamba hakuna takwimu juu ya harakati za ugaidi katika nchi hiyo, na yule adui anayetafutwa hajulikani ni yupi na yuko wapi. Mara hii Magazeti ya India, yakiwa na vichwa vya habari kama vile YATOSHA YATOSHA, yameripoti kwamba kulikuweko maonyo ya kutosha hapo kabla kwamba janga hilo litatokea. Sasa serekali kuu ambayo mwakani itabidi iombe kura za wananchi ili ibakie madarakani, iko katika shinikizo kubwa, na suala ni kama serekali hiyo itaweza kwa muda mrefu ujao kuustahamilia mbinyo huo kwa kuelekeza tu lawama kwa nchi jirani ya Pakistan. Waziri wa mambo ya kigeni wa Pakistan, Shah Mehmood Qureshi, anatambuwa kwamba mambo ni ya hatari:
"Bila ya shaka, hali ya mambo ni ngumu, tusijidanganye. Pale jirani yetu au wananchi wakiwa na hisia kwamba yaliotokea ni kama yale yaliotokea Marekani, Septemba 11, 2001, na wanasema hivyo, basi hali ya mambo ni ngumu."
India haijasema kwamba Pakistan ni dhamana moja kwa moja ya mashamnbulio ya Mumbai, lakini kuna watu ndani ya Pakistan wanaobeba dhamana hiyo. Na jambo hilo lilihakikishwa na gaidi pekee aliyebakia hai na kukamatwa, pale alipokiri kwamba ametokea Pakistan, amepata mafunzo huko, na kwamba yeye na wenzake hawajakuwa tu na nia ya kuiripuwa hoteli ya Taj Mahal, lakini wao ni wanachama wa kikundi cha kigaidi cha Waislamu, Lashka-e-Toiba, lenye maana jeshi la walio wasafi. Makundi kama hayo, ambayo yako karibu 16 au 17 hivi, yanapigana na serekali ya India na hayataki nchi mbili jirani za India na Pakistan ziwe na uhusiano wa kawaida. Makundi hayo yamekuwa na maingiliano na idara ya ujasusi ya serekali ya Pakistan, ISI. Lakini waziri wa mambo ya kigeni wa Pakistan alihakikisha:
"Pakistan imeazimia kikweli kupambana na ugaidi katika sura zake zote. kwani sisi pia ni wahanga wa ugaidi."
Ni nia ya Marekani kwamba madola ya kinyukliya ya India na Pakistan yaelekeze nguvu zao katika kupambana na ugaidi na yasitumie nguvu hizo katika kuzidisha tafauti baina yao. Kwani, kwa Wamarekani, itakuwa ni jambo la kutisha pale majeshi ya nchi zo mbili yatakapopambana katika mpaka wao wa pamoja, na kupelekea Pakistan iondoshe majeshi yake kutoka mpka wake na Afghanistan. Hapo tena wenye siasa kali wataifurahia hali hiyo. Hivi sasa kuna wanajeshi laki moja wa Pakistan katika mpaka huo wakiyasaidia majeshi ya Kimarekani na washirika wake katika vita dhidi ya ugaidi. Kwa vyovyote, hali ya hewa sasa sio nzuri katika uhusiano baina ya New Delhi na Islamabad.
Isisahaulike kwamba India na Pakistan zimepigana mara tatu tangu zilipopata uhuru mwaka 1947. Mwaka 2001, baada ya shambulio la magaidi dhidi ya jengo la Bunge huko New Delhi zilikuwa karibu ziingie vita vya nne. Hadi hivi karibuni pande zote mbili zimejaribu kuyatanzuwa matatizo ya ugaidi na ya mizozo ya ardhi kwa njia ya ushirikiano. Lakini shambulio la wiki iliopita huko Mumbai litazirejersha nyuma juhudi hizo. Rais Asif Ali Zardai wa Pakistan amesisititza kwamba India isipandishe mori, na kuna hatari kwamba siasa za ndani za India zitaipalilia hali hiyo. Katika baadhi ya mikoa kunafanyika hivi sasa chaguzi, na mwakani uchaguzi wa bunge la nchi nzima.Chama cha wazalendo wa kibaniani, BJP, kinawachochea wanachama wake wachukuwe msimamo mkali dhidi ya serekali na kinainyoshea kidole serekali ya Islamabad kwa yote yaliotokea. Hivyo haijawa ajabu kwa waziri mkuu wa India, Manmohan Singh, naye kulaumu kwamba nchi za nje, na hivyo kumaanisha Pakistan, zinawaachia Waislamu wenye siasa kali kuingia India kuleta vurugu.
Pia isikatalike kwamba serekali ya New Delhi imezubaa kuyaangalia maslahi ya Waislamu walio wachache katika nchi hiyo. Waislamu wa India ndio walio maskini zaidi kuliko wakaazi wengine,wasiojuwa kusoma na kuandika na wasiokuwa na kazi miongoni mwao ni wengi zaidi uliinganisha na watu wa dini nyingine. Katika utumishi wa serekali hawana uwakilishi mkubwa. Pia wamekuwa wakishambuliwa na mabaniani wenye siasa kali. Mauaji waliofanyiwa katika jimbo la Gujarat yalichukuwa maisha ya watu wao zaidi ya alfu moja, na hakuna hata kiongozi mmoja wa kibaniani aliyechochea mauaji hayo amefikishwa mahakamani. Waziri kiongozi wa Gujarat, Narendra Modi, aliyawachia mauaji hayo, bila ya kuyazuwia, hadi leo yuko madarakani. Hali hiyo inaleta mivutano na wenye siasa kali wanapata cha kusema.
Mnamo miaka minne iliopita kumepatikana maendeleo katika kukaribiana baina ya India na Pakistan, nchi mbili zilizo na uhasama wa jadi. Mawasiliano ya safari za mabasi na gari moshi yameanzishwa na pia biashara imekuwa ikifanyika hata kupitia eneo la mzozo la Kashmir. Nchi hizo mbili zimebadilishana wafungwa na zimeahidi kushirikiana zaidi katika kupambana na ugaidi.
Mtu mmoja huko Pakistan alihuzunika juu ya kulaumiana kulioko baina ya nchi hizo mbili jirani:
"Ni mambo yale yale kutoka kwa wanasiasa wetu. Hawashughuliki juu ya maslahi ya taifa, wana mambo waliojiwekea wao mbele. Mtu wa kawaida afanye nini? Hata akiwa na fikra nzuri, fikra hizo hazitakuwa na athari nje ya kuta nne za chumba chake."
Na mwanamke mmoja alisema ugaidi hauhusiani na dini:
" Bila ya shaka, sisi sote tuna huzuni. Kwani katika Uislamu hakuna haki ya kuhatarisha au kuyamaliza maisha ya mtu asiyekuwa na hatia. Ni makosa na haitakiwi kufanyika."