Mashirika: Mwaka wa tano wa vita vya Syria ndio mbaya zaidi
11 Machi 2016Takriban watu 50,000 waliuawa, milioni moja na laki tano walihitaji kwa dharura misaada ya kibinadamu na karibu milioni moja ya Wasyria walilazimika kuyatoroka makaazi yao mwaka jana.
Ripoti iliyotolewa na mashirika hayo ya kimataifa na ya Syria imesema huku pande zinazozana zikiendelea kupigana, misaada zaidi ikishindwa kuwafikia watu na jamii zaidi zikizingirwa, Wasyria wamezidi kuteseka sana.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa nyumba laki mbili zimeharibiwa Syria hiyo ikiwa ni asilimia 20 zaidi ya hali ilivyokuwa mwaka 2014. Mwaka jana, watoto laki nne zaidi waliacha shule na hivyo kufikisha idadi ya watoto wasiopata elimu kufikia milioni mbili.
Katika ripoti yake iliyopewa jina 'Kuuchochea Moto', mashirika ya kutoa misaada ya kibianadamu yakiwemo Oxfam, Action Aid, Save The Children, CARE Intenational na mashirika kadhaa ya Syria yamesema yanaamini baadhi ya nchi wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia zimehujumu wajibu wao kuhusu Syria.
Licha ya kuwa mashirika hayo yamesema makubaliano ya kusitisha mapigano yanazingatiwa katika sehemu kadhaa nchini humo tangu tarehe 27 mwezi uliopita, maazimio yaliyopitishwa na Baraza la Usalama yamekuwa yakikiukwa na pande zinazozana.
Ripoti hiyo pia imezitaja nchi hizo wanachama wa Baraza la Usalama kuwa kutokana na hatua zao za kijeshi za moja kwa moja, zimeongeza mafuta katika moto wa mzozo wa Syria.
Mashambulizi ya angani yanayofanywa na Urusi tangu mwezi Septemba mwaka jana yamelenga miundo mbinu inayotumiwa na raia na kuiharibu huku pia vifo vya raia kutokana na mashambulizi hayo ya Urusi vikiripotiwa.
Vile vile, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani pia umesababisha vifo vya raia na uharibifu wa maeneo ya makaazi na pia unashutumiwa kwa kusafirisha moja kwa moja silaha kwa makundi mbali mbali ya wapiganaji wa upinzani.
Ufaransa na Uingereza ambazo zilijiunga na muungano huo wa kijeshi baadaye ili kufanya mashambulizi ya angani pia zimeshutumiwa kwa kutumia mamilioni ya dola kununua silaha.
Ripoti hiyo ya kurasa 33 pia imesema mashirika ya kutoa misaada yalipata tabu mwaka jana kuwasilisha misaada katika maeneo yanayozingirwa na mashambulizi yaliyovilenga vituo vya afya yaliongezeka kwa asilimia 44.
Ripoti hiyo imesema wahusika wote zikiwemo serikali zinazokaa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimehusika moja kwa moja katika athari ambazo vita vya Syria zimesababisha.
Mashirika hayo yanazitaka kila pande kuhakikisha ghasia na mateso vinakomeshwa na kuchangia kikamilifu katika kupatikana amani ya kudumu.
Tangu vita hivyo kuanza, zaidi ya nusu ya idadi ya Wasyria wamelazimika kuyahama makaazi yao na zaidi ya watu laki mbili na elfu hamsini wameuawa.
Mzozo wa Syria ulianza kama maandamano ya amani dhidi ya utawala wa Rais Bashar Al Assad na kugeuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mwandishi: Caro Robi/dpa/www.dw.com/en
Mhariri:Josephat Charo