Mashirika ya UN yaonya kuhusu njaa kali Somalia
7 Juni 2022Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema kiasi robo milioni ya watu wanakabiliwa na njaa kali nchini Somalia. Hali hiyo imesababishwa na ukame unaozidi kuwa mbaya pamoja na ongezeko la bei ya vyakula duniani.
Tamko lililotolewa kwa pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa,WFP ambalo linahusika na mpango wa chakula duniani, lile la chakula na kilimo FAO na lile linaloshughulikia masuala ya watoto UNICEF pamoja na ofisi ya kuratibu shughuli za msaada wa kibinadamu katika Umoja wa Mataifa OCHA inaonesha kwamba kiasi wasomali 213,000 wako hatarini kutumbukia kwenye njaa,idadi ambayo imeongezeka mara dufu ikilinganisha na idadi iliyotarajiwa mwezi Aprili.
Mashirika hayo yameeleza kwamba mvua haikunyesha kwa misimu minne mfululizo kwenye eneo hilo la upembe wa Afrika na watabiri wa hali ya hewa wanatahadharisha kwamba msimu mwingine unaokuja mwishoni mwa mwaka huu,hautakuwa na mvua za kutosha.Hali hiyo inashuhudiwa katika wakati ambapo hali ya hewa ya ulimwengu haiwezi kutabirika.
Dunia iko kwenye mfumko wa bei
Wakati huohuo dunia pia inashuhudia mfumko mkubwa wa bei ya vyakula ambapo mwezi March bei zilifikia rekodi ya juu wakati vita kati ya Urusi na Ukraine vikiathiri masoko ya mazao ya nafaka na mafuta ya kupikia.Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwahivyo yanasema takriban wasomali milioni 7.1 ambao ni kiasi nusu ya idadi jumla ya wakaazi wa nchi hiyo wanakabiliwa na kiwango kikubwa cha ukosefu wa usalama wa chakula,ikimaanisha kwamba idadi hiyo ya watu watashindwa kupata vyakula wanavyohitaji na huenda wakalazimika kuuza mali zao ili kukidhi mahitaji hayo na kuishi.
Mkurugenzi wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP,nchini Somalia.El-Khidir Daloum amesema watu wengi walioko hatarini tayari wanakabiliwa na kitisho cha utapiamlo na njaa na kwahivyo hawawezi kutazama na kusubiri mpaka wafikie kutangaza kuna njaa ili hatua zichukuliwe. Mpaka sasa mashirika hayo yanasema kiasi mifugo milioni 3 imeshakufa nchini Somalia kufuatia ukame tangu katikati ya mwaka 2021.
Mpango wa kushughulikia masuala ya kiutu wa Umoja wa Mataifa wa mwaka huu unadhaminiwa kwa asilimia 18 tu mpaka sasa na Somalia sio nchi pekee inayokabiliwa na matatizo kuna nchi nyingine nyingi duniani ambazo zinahitaji msaada wa dharura katika kipindi ambacho njaa inashuhudiwa ikisambaa kote duniani.
Mnamo mwaka 2011 njaa ilisababisha kiasi robo ya watu kufariki nchini Somalia.Hivi sasa mashirika hayo yanasema watu wasiopungua milioni 7.1 hawana chakula lakini hali ni mbaya zaidi kwa watu 213,000 ambao wameathirika kwa kiasi kikubwa sana na wanahitaji kwa dharura msaada.Ukame unaolikumba eneo hilo la Upembe wa Afrika haujawahi kutokea kwa kipindi cha miaka 40 iliyopita na mgogoro mkubwa wa njaa unaziandama pia Kenya,na Ethiopia.
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed Khelef