Masuala ya migogoro na amani yatawala Umoja wa Mataifa
26 Septemba 2019Suala la Iran lilipewa kipaumbele. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya kwamba dunia inakabiliwa na uwezekano wa kutokea vita katika Ghuba ya Uajemi, ambavyo havitoweza kuvumiliwa.
Shambulio la hivi karibuni dhidi ya vituo vya mafuta vya Saudi Arabia, ambalo Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zinadai Iran imehusika limezidisha hali ya wasiwasi.
Iran kwa upande wake inakana madai hayo. Rais wa Iran Hassan Rouhani katika hotuba yake ameikosoa Marekani kwa kuchochea vita Syria, Yemen na Afghanistan. Rouhani pia amesema hayuko tayari kufanya mazungumzo na Rais Donald Trump wa Marekani hadi pale nchi hiyo itakapoviondoa vikwazo vibaya zaidi katika historia dhidi ya Iran.
"Kwa niaba ya taifa langu pamoja na serikali, ningependa kutangaza kwamba hatukubali kuitika mazungumzo yoyote chini ya vikwazo," amesema Hassan Rouhani.
Soma zaidi: Siku ya pili ya kikao cha hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa
Naye rais wa Iraq Barham Saleh, ambaye nchi yake imekwama katika mgogoro wa mahasimu wawili wa kikanda Iran na Saudi Arabia, amesema hatokubali kuiona nchi yake inageuzwa uwanja wa kupigana vita vya nchi nyingine.
Rais wa Lebanon Michael Aoun ambaye nchi yake inahifadhi wakimbizi wa Syria amewatolea wito viongozi wa dunia kuwasaidia mamia kwa maelfu ya wananchi wa Syria kurudi nyumbani kwa salama walikokimbia vita vya miaka minane.
Migogoro ya Afrika
Rais mpya wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kwa mara ya kwanza alizungumza mbele ya Hadahara Kuu ya Umoja wa Mataifa na kuzungumzia maafa yanaoytokana na mgogoro unaoendelea kati ya nchi yake na Urusi. Zelenskiy amesema Ukraine inataka kupata amani kwa njia ya kistaarabu.
Kwa upande wa Afrika, mgogoro mbaya zaidi wa tangu 2013 kati ya upande wa serikali na makundi ya uasi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati pia ulijadiliwa. Rais wa nchi hiyo Faustin Archange Touadera amesema hali bado ni tata licha ya juhudi za serikali kutaka kudhibiti maeneo zaidi nchini humo na kufanya mabadiliko katika sekta ya usalama na ulinzi.
Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amezitolea wito Marekani na nchi za Ulaya kuondoa vikwazo alivyovitaja kuwa ni kinyume cha sheria ilivyowekewa nchi yake na ambavyo vinaizuia kuimarika kiuchumi.
ap,ape,afpe