Mataifa ya Afrika yahimizwa kuongeza upimaji wa covid-19
21 Mei 2020Mkurugenzi wa kituo cha Afrika cha kudhibiti na kuzuwia mgonjwa (Afrika-CDC) John Nkensong anasema Afrika inapaswa kujitahidi kupima angalau asilimia moja ya wakazi wake bilioni 1.3, au watu milioni 13, lakini mpaka sasa ni vipimo milioni 1.3 au 1.4 tu vilivyofanywa.
Idadi ya visa vya mambukizi barani Afrika ni zaidi ya 95,000 na inaweza kupindukia 100,000 kufikia mwishoni mwa wiki. Bara hilo limeshuhudia karibu idadi sawa ya visa katik muda wa wiki iliyopita kama ilivyokuwa wiki iliyotangulia, na Nkengasong anasema kwamba "tunatumaini mwelekeo huo unaendelea."
Wakati hatua za mapema za kufunga shughuli zimechelewesha janga hilo, anasema "hilo halimanishi Afrika imenusurika." Lakini anasema maafisa wa afya hawashuhudii vifo vingi katika jamii au "kufurika kwa hospitali zetu" kwa sababu ya Covid-19.
Mataifa yalio na mifumo dhaifu ya kiafya na historia ya karibuni ya migogoro kama vile Somalia na Sudan Kusini hata hivyo, yanasalia kuwa yanayotia wasiwasi wakati ambapo idadi ya visa inapanda haraka.
Somalia imeripoti zaidi ya visa 1,500 lakini mashirika ya misada yana wasiwasi kwamba idadi halisi ni kubwa zaidi. Sudan Kusini ina visa zaidi ya 280.
Wanasayansi Afrika Kusini wasema vifo hadi 50,000 vinaweza kutokea
Ruwaza za kisayansi nchini Afrika Kusini zimeonyesha siku ya Alhamisi kuwa nchi hiyo inweza kushuhudia hadi vifo 50,000 kutokana na virusi vya corona na maambukizi yanaweza kufikia milioni 3 kufikia mwishoni mwa mwaka, wakati majira ya baridi ya nusu ya kusini ya dunia yakisababisha viwango vikubwa vya mambukizi.
Nchi hiyo tayari ndiyo ina idadi kubwa zaidi ya visa vya mambukizi na vifo barani, ikiwa na kesi zilizotambuliwa 18,000 na vifo 339, lakini hatua za kitaifa za kufunga shughuli zinazoingia katika wiki yake ya sita zimepunguza kasi ya mambukizi.
Hata hivyo wanasayansi na wataalamu wa takwimu walioajiriwa n wizara ya fya kuchora ruwaza ya mambukizi ya ugonjwa huo wamesema nchi inaweza kushuhudia kati ya vifo 35,000 na 50,000 vinavohusiana na coron kufikia mwezi Novemba.
"Bado hatujaweza kusawazisha kizingo," alisema moja wa wataalamu, Martin Moultrie, katika uwasilishaji ulioonyeshwa kwenye runinga. "Pia tuna wasiwasi mkubwa kwamba kwa sababu ya kuweka nadhari kwenye covid-19, hili linaweza kuhatrisha maeneo mengine kama vile VVU na Kifua Kikuu.
Ruwaza hizo, zinazozingatia mazingira bora na mabaya zaidi, zinaonesha uwezekano wa kuwa na visa hadi milioni 2 vya virusi vya corona kufikia Novemba, huku mahitaji ya vitanda vya hospitalini yakionekana kufikia kilele kwa 45,000, karibu mara kumi ya vitanda vilivyopo sasa vya magonjwa mahututi.
Ruwaza moja ilionyesha vizuwizi vimepunguza kiwango cha maambukizi kwa asilimia 60, na kwamba tangu mwanzoni mwa mwezi Mei, wakati masharti ya vizuwizi yalivyolegezwa, kiwango hicho kimepungua hadi asilimia 30.
"Kwa hatua za kufunga shughuli tulikuwa tunaweka kizuwizi kinachozuwia virusi kusambaa," alisema waziri wa afya Zweli Mkhize. "Vizuwizi vilikuwa na thamani makhsusi. Sasa tunajaribu kusonga mbele na mkakati tofauti kidogo, ambao umebadilishwa kihatari."
vyanzo: ape,rtre