1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yapambana kudhibiti COVID 19

15 Desemba 2020

Kutoka Asia hadi Ulaya, Marekani hadi Afrika, wimbi jengine la maambukizo ya virusi vya corona linaripotiwa kuanza rasmi na tayari idadi ya watu walioambukizwa na kupoteza maisha inatajwa kupanda kwa kasi. 

https://p.dw.com/p/3mjhG
Moon Jae-in Präsident Südkorea
Picha: South Korea Presidential Blue House via AP

Kutoka Asia hadi Ulaya, Marekani hadi Afrika, wimbi jengine la maambukizo ya virusi vya corona linaripotiwa kuanza rasmi na tayari idadi ya watu walioambukizwa na kupoteza maisha kutokana na ugonjwa wa COVID-19 inatajwa kupanda kwa kasi. 

Korea Kusini tangu Januari ilifanikiwa pakubwa kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona kutokana na hatua zake za kuwataka raia kuvaa barakoa na kuwazuia kusafiri lakini pia ikizuia watu kwenda kwenye mikusanyiko.

Hata hivyo, taasisi ya kitaifa ya kudhibiti magonjwa ya KDCA imeripoti rekodi mpya ya maambukizi ya kila siku iliyofikia visa 1,030 juzi Jumapili na 718 jana Jumatatu.

Moon Jae In amesema kwenye hotuba hiyo kwamba huu ni wakati muhimu kabisa kwa watu wa taifa hilo kwa ujumla kujitoa kwa dhati na kwa uwezo wao wote kuzuia kusambaa zaidi kwa virusi hivyo, akiongeza kuwa wako katika wakati mgumu mno.

Kuanzia leo, shule za mjini Seoul na maeneo jirani zitafungwa na wanafunzi watasoma kwa njia ya mtandao hadi mwishoni mwa mwezi huu, huku watumishi wa huduma za muhimu tu wakiruhusiwa kwenda ofisini na mikusanyiko itakakayoruhusiwa ni ya watu chini ya 10.

Niederlande Premierminister Mark Rutte
Mark Rutte ameonya kwamba ni lazima kuchukuliwe hatua kali ili kuzuia kusambaa zaidi kwa virusi vya corona.Picha: Remko De Waal/ANP/picture alliance

Hapa barani Ulaya, huko Uholanzi waziri mkuu Mark Rutte ametangaza vizuizi vikali kwa kufunga kabisa shughuli ili kukabiliana na kusambaa zaidi kwa virusi vya corona hadi Januari 19. Rutte ataangazia upya hali ilivyo na Januari 12 atatangaza iwapo vizuizi hivyo vitaondolewa ama vitasalia.

Kwenye hotuba yake kupitia televisheni, Rutte amesema chini ya vizuizi hivyo maduka ya bidhaa zisizo za muhimu yatafungwa, pamoja na bar, majumba ya sinema, makumbusho na bustani za wanyama. Shule za msingi na sekondari pia zitafungwa na watoto watasoma kupitia mitandao.

"Chini ya wiki moja iliyopita nilisema tulikuwa njia panda. Kisha nikasema hatua kali zitakuwa chaguo ikiwa kiwango cha maambukizi kitapanda. Kwa bahati mbaya hiyo ndio tunayoona ikitokea kwa kasi sana. Ndio maana Uholanzi itafunga shughuli kwa angalau wiki tano. Uholanzi itafungwa. Hii inamaanisha tutafunga sehemu zote ambazo watu hukusanyika. Yote haya ni kwa lengo la kupunguza watu kukutana. Kwa sababu virusi haviwezi kueneo iwapo watu hawatakutana." alisema Rutte.
 

USA Washington. Donald Trump
Rais Donald Trump aelezea furaha yake baada ya kuanza kutumika chanjo dhidi ya virusi vya corona.Picha: Yuri Gripas/ZUMA Wire/imago images

Trump ashangilia kuanza kutolewa chanjo dhidi ya virusi vya corona.

Huko nchini Marekani, tayari taifa hilo limeanza kusambaza dozi za mwanzo za chanjo dhidi ya COVID 19 yaBioNTech-Pfizer hapo jana, siku chache baada ya kuthibitishwa na mamlaka ya chakula na dawa, FDA.

Sandra Lindsay, muuguzi kutoka New York alikuwa wa kwanza kupata chanjo na kuzindua rasmi mchakato huo.

Makamu wa rais wa idara ya utafiti na uvumbuzi katika chuo kikuu cha Virgini Tech Lisa Lee ameliambia shirika la habari la DW kwamba ilikuwa ni hatua kubwa kumuona muuguzi yule akipata chanjo na kuashiria kuanza rasmi kwa programu hiyo nchini Marekani, huku akionyesha matarajio chanya ya huko siku za usoni.

Rais Donald Trump amezungumzia hatua hiyo kwa furaha na kuandika kwenye ukurasa wake wa Twitter "hongera Marekani", "hongera Ulimwengu"

Mashirika: DW