1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yajitenga na tamko la mwanasiasa wa DRC

17 Desemba 2023

Corneille Nangaa atangaza akiwa Nairobi,kuunda muungano wa kijeshi wenye malengo ya kisiasa,utakaolijumuisha kundi la M23 kuipinga serikali ya Kongo

https://p.dw.com/p/4aGoJ
Corneille Nangaa, ehemaliger chef der Wahlkommission (Céni) im Kongo
Picha: John Wessels/AFP

Kenya imejitenga na tamko lililotolewa na mwenyekiti wa zamani wa tume ya uchaguzi ya Kongo,Corneille Nangaa ambaye siku ya Ijumaa alitangaza kuunda muungano wa kijeshi wenye malengo ya kisiasa pamoja na kundi la waasi la M23 na makundi mengine yenye silaha nchini humo.

Wizara ya mambo ya nje ya Kenya leo Jumapili imesema haina mahusiano yoyote na mwanasiasa huyo wa Kongo na kujitenga kabisa na tamko lake ambalo limezusha mvutano wa kidoplomasia kati ya serikali ya Kinshasa na Kenya.

Cornnelle Nanga alitangaza kuunda muungano huo wa kijeshi na kisiasa akiwa katika hoteli moja jijini Nairobi na hatua yake hiyo ukazusha ghadhabu na matamshi makali kutoka serikali ya Kongo,ikiionya Kenya kujindaa kukabiliwa na kile ilichokiita,athari za kumkaribisha mwanasiasa huyo.

Corneille Nangaa, aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini Kongo-CENI
Corneille Nangaa, mwenyekiti wa zamani wa CENI akizungumza na waandishi habariPicha: Luis Tato/AFP

Waziri wa mambo ya nje wa Kenya Musalia Mudavadi kupitia taarifa aliyoitowa,amesema Kenya inajitenga na matukio au matamshi yoyote yenye uwezekano wa kuvuruga amani na usalama wa nchi ya Kongo ambayo ameiita ni rafiki wa Kenya.Kwa mujibu wa Mudavadi,uchunguzi umeanzishwa kubaini waliotowa matamshi hayo ambayo yalikwenda mbali zaidi na kukiuka misingi ya katiba.

Pamoja na hilo,waziri huyo wa mambo ya nje wa Kenya alitetea msimamo wa nchi yake akisema kuna uhuru wa vyombo vya habari na mtu yoyote yuko huru kuzungumza na vyombo vya habari bila ya kuitaja serikali.

Tamko la Corneille Nangaa la kuunda muungano wa kijeshi wenye malengo ya kisiasa ambao utajumuisha makundi kiasi tisa ya waasi ikiwemo M23 limekuja katika wakati ambapo mazingira ya kisiasa nchini mwake Kongo ni ya wasiwasi mkubwa huku ikijiandaa kufanya  uchaguzi wa rais Desemba 20.

Kundi la waasi wa Ma23 wakilinda eneo la Rumagangabo,Kongo
Kundi la waasi wa Ma23 wakilinda eneo la RumagangaboPicha: Guerchom Ndebo/AFP

Nangaa aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi mwaka 2018 amehalalisha hatua yake ya kuunda muungano huo kwa kusema inatokana na kile alichokiita udhaifu wa serikali ya Kongo ulioonekana katika kipindi cha miongo mitatu pamoja na kushindwa kwake kurudisha mamlaka thabiti nchi nzima.Amedai kwamba muungano huo unalenga kulea mshikamno wa taia na uthabiti.

Serikali ya Kongo hata hivyo imeilaani hatua ya Nangaa ikiita sio ya kizalendo na kuahidi kuichukulia hatua za kidiplomasia Kenya kwa kumkaribisha nchini humo.Serikali ya Kongo pia ilimuhoji balozi wa Kenya mjini Kinshasa jana Jumamosi huku pia ikiwaita nyumbani mabalozi wake walioko Nairobi kwa mashauriano

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW